Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba akifungua kikao kazi cha wadau wa elimu waliokutana mjini Morogoro hivi karibuni kwa lengo la kupitia Rasimu ya Mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa BOOST unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Tume ya Utumishi wa walimu (TSC) inafanya kikao na wadau mbalimbali wa elimu kwa lengo la kupitia na kufanya maboresho ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa BOOST unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Akizungumza katika kikao kazi hicho kilichowakutanisha wadau wa elimu kwa siku nne kuanzia Januari 10 - 13, 2023 mjini Morogoro, Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba amesema TSC inamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona suala la maadili ya walimu linahitaji kupewa kipaumbele na kuamua sehemu ya fedha za mradi wa BOOST zielekezwe kwenye eneo hilo.
“Tume ya Utumishi wa Walimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu tunamshukuru sana Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona maadili ya walimu ni moja ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele katika mradi huu wa BOOST. Maadili ya walimu ni muhimu kwa kuwa mwalimu ndiye anayemtengeneza mwanafunzi kuwa raia mwema au raia asiyefaa katika jamii,” alisema Prof. Komba.
Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu ambao Rais aliuonesha katika eneo hilo, TSC ina jukumu kubwa kuhakikisha inasimamia walimu kwa karibu na kuwakumbusha mara kwa mara kuzingatia taratibu na miiko ya taaluma hiyo katika kuwalea wanafunzi.
Prof. Komba aliendelea kueleza kuwa kwa kiasi kikubwa walimu wamejikita zaidi katika kufundisha wanafunzi masomo ya darasani na kuhakikisha wanafaulu katika mitihani yao huku wakisahau kujenga wanafunzi katika maadili mema yanayowaandaa kuwa raia wema katika jamii na Taifa kwa ujumla.
"Mwanafunzi asiyekuwa na Maadili hata akifaulu vizuri haina maana. Mwanafunzi anaweza kupata Daraja la kwanza lakini akiingia mtaani anakuwa mwizi, mla rushwa, mtu asiye na heshina, mtumia madawa ya kulevya, nk, hapo taaluma yake haina maana kwa kuwa anakuwa ni hasara kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Hivyo, suala la maadili ni jambo muhimu sana katika taaluma ya Ualimu," alisema Prof. Komba.
Prof. Komba pia aliongeza kuwa suala la kufanya ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu ni muhimu litasaidia kuelezea kanuni hizo katika lugha rahisi ambayo itafanya walimu kuielewa na kuzingatia maadili hayo katika utendaji kazi wao, hivyo aliielekeza Sekretareti ya Tume hiyo kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa weledi na ufanisi ili kufikia malengo yaliyotarajiwa.
Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo aliiagiza Sekretarieti ya Tume hiyo kuhakikisha inatoa elimu kwa walimu na wadau wengine kuhusu ufafanuzi wa Kanuni hizo ili kuwasaidia walimu kujiepusha na ukiukwaji wa maadili ya kazi yao kitu ambacho kinasababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
Akitoa neno la utangulizi, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama amesema Tume imewezeshwa kufanya mapitio ya Kanuni za Maadili na Miiko ya kazi ya Ualimu ili kutoa ufafanuzi wa kanuni hizo ziweze kueleweka kirahisi na watumiaji ambao ni walimu.
“Tume ya Utumishi wa Walimu chini ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI ni watekelezaji wa shughuli za Mradi wa BOOST ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo katika utekelezaji wa shughuli za Mradi huo, Tume imewezeshwa, kununua vitendea kazi vikiwemo Kompyuta na Magari pamoja na kujengea uwezo watumishi wa TSC kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.”
“Napenda kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwa na Miradi ya Maendeleo ambapo leo Tume kupitia Mradi wa BOOST imeweza kufanikisha kwa sehemu kubwa utekelezaji wa majukumu yake.”
“Ninapenda kumpongeza pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Katibu Mkuu kwa kuona umuhimu wa Tume kuwezeshwa na Mradi huo ili kutekeleza majukumu yake ambayo moja kwa moja yanamlenga Mwalimu kwa ajili ya kuleta matokeo chanya kwa mwanafunzi shuleni, pia ninawashukuru Benki ya Dunia ambao wanasimamia utekelezaji wa Mradi kwa kuridhia Tume kuwa watekelezaji wa shughuli za Mradi,” alisema Nkwama.
Alieleza kuwa Mradi wa BOOST utekelezaji wake umejikita katika Afua nane ikiwemo Afua ya Mpango wa Shule Salama na kueleza kuwa Mwalimu anayezingatia Maadili na Miiko ya kazi yake ana mchango mkubwa katika kuifanya Shule iwe salama, hivyo, kupitia Mradi huo, Tume imezeshwa kufanya mapitio ya Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu na kuandaa rasimu ambayo imewasilishwa katika kikao kazi hicho kwa ajili ya kupata maoni ya wadau.
Kwa mujibu wa Nkwama, kumekuwa na ongezeko la baadhi ya walimu wanaojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili ya kazi ya ualimu na hivyo kufanya kazi ya ualimu ipoteze hadhi yake, hivyo TSC ambayo ni mamlaka katika kumsimamia Mwalimu kwa mujibu wa Sheria Sura 448 imeona iangalie kwa upya Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu ili kuweka Mikakati ya kuitekeleza na hatimaye kutimiza azma ya Serikali ya kuwa na Mpango wa Shule salama.
Naye Kamishna wa TSC, Jane Mtindya amesema kuwa katika jamii ya sasa ya utandawazi, taarifa zinaenea kwa kasi zaidi tofauti na miaka ya nyuma hivyo ni vyema kuwakumbusha walimu wetu ili wawasaidie kuwa na tabia ya kuzingatia mambo yenye tija kwao na kwa taifa badala ya kuiga tabia ambazo ni kinyume na maadili ya Kitanzania.
“Katika dunia tunamoishi taarifa zinasambaa kwa kasi sana na cha kusikitisha taarifa mbaya zilizo kinyume na maadili yetu ndizo zinazo samba zaidi hususani kwa vijana. Hivyo, kazi hii ya kufafanua Kanuni za Maadili na utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu ni muhimu katika kuwasaidia walimu wafanye wajibu wao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuwalea wanafunzi katika maadili mema,” alisema.
0 Comments