Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Subisya Kabuje akiongoza timu ya Spark Health Afrika na TECDEN kutembelea wataalam wa afua za Mpango za Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika Halmashauri ya Bahi, Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Subisya Kabuje akiongoza timu ya Spark Health Afrika na TECDEN kutembelea wataalam wa afua za Mpango za Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika Halmashauri ya Kongwa, Dodoma.
Mkurugenzi wa Programu kutoka Taasisi ya Spark Health Africa, Tendai Gotora akifafanua jambo wakati wa ziara wilayani Bahi kwa ajili ya kujionea utekelezaji wa afua za Mpango wa Malezi Mkuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(ECD) kufuatia mafunzo ya uongozi wa mabadiliko kwa uratibu madhubuti.
Na Mwandishi wetu, DODOMA
MAFUNZO ya uongozi wa mabadiliko kwa uratibu madhubuti wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika ngazi za mitaa yameanza kuleta matunda kwa kuharakisha utekelezaji wa programu hiyo.
Mafunzo hayo yalitolewa na Spark Health Africa kwa kushirikiana na Mtandao wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Watoto Wadogo Tanzania (TECDEN), ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuharakisha utekelezaji wa mpango huo.
Mradi wa miezi 18 wa Spark Health Africa, unaofadhiliwa na Hilton Foundation, unalenga kukuza uongozi wa mabadiliko na mabadiliko ya kiutamaduni katika ngazi ya halmashauri, hususan katika Halmashauri za Bahi, Chamwino, Kongwa na Dodoma Mjini mkoani Dodoma, kwa lengo la kubadili namna huduma kwa watoto wadogo zinavyoratibiwa na kutolewa.
Akizungumza mara baada ya ziara ya tathmini, Mratibu wa Mradi, Profesa Mshiriki (Associate Professor) Fortidas Bakuzza, alisema mafunzo hayo yalitolewa mwaka 2024 na 2025 katika ngazi ya taifa, mkoa na halmashauri, na yameanza kuleta matunda katika kumhudumia mtoto.
“Tumeona mabadiliko makubwa sana. Timu za kisekta zinafanya kazi kwa kushirikiana, jambo ambalo si la kawaida. Kwa pamoja wanamhudumia mtoto na kuwa na mipango ya pamoja. Mafanikio ni makubwa na changamoto ni chache. Kila mafanikio yana changamoto zake, lakini wanaweza kuziboresha kadri muda unavyoenda. Sisi tumeridhika,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu kutoka Taasisi ya Spark Health Africa, Tendai Gotora, alipongeza kazi iliyofanywa na wataalamu hao na kuhimiza umuhimu wa kutumia takwimu katika taarifa zao.
“Takwimu ni kama kioo. Hivyo, ukitaka kuona kama unapiga hatua au la, ni vema mkazingatia matumizi ya takwimu sahihi. Hata hivyo, kazi nzuri imefanyika,” alisema.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Subisya Kabuje, alisema Tanzania iko katika nafasi nzuri katika utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
Aliwataka wataalamu wa sekta zinazohusika na afua za mtoto kutekeleza wajibu wao ili kuendelea kufanya vizuri zaidi kama nchi.
“Kwenye utekelezaji wa afua za Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto, kama nchi tuko pazuri. Lakini tunatakiwa kufanya vizuri zaidi, hasa ukizingatia kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara wa masuala ya lishe. Anazungumzia vituo vya kulelea watoto masokoni na hivi karibuni ameteuliwa kuwa Balozi wa Mama na Mtoto Afrika. Haya yote yanamhusu mtoto,” alisema. Kabuje alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wa Spark Health Africa na TECDEN kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa ngazi ya halmashauri, hatua ambayo imesaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa afua za mtoto.
Naye mwakilishi wa Mtandao wa TECDEN, Merina Maneno, aliwataka kubainisha hatua walizozipiga kwa kuainisha viashiria vya utekelezaji wa mpango huo, sambamba na kuweka bayana bajeti iliyotumika wakati wa kutekeleza afua za mtoto.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Maria Haule, alisema kwa sasa halmashauri imekuwa ikiweka mbele utengaji na utoaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za mtoto.
“Siku za nyuma fedha zote zilikuwa zinakuja Idara ya Afya, ambayo ndiyo ilikuwa inapanga shughuli za mtoto bila kushirikisha idara nyingine. Lakini sasa Mkurugenzi wa Halmashauri anatoa fedha za afua za mtoto katika kila idara. Tumetenga shilingi milioni 1.8 zaidi ya kiwango kilichowekwa na Serikali, na kwa robo ya pili tumetumia shilingi milioni 38,” alisema.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Elimu ya Awali na Msingi, Agatha Ntandu, alisema kabla ya mafunzo kila idara ilikuwa ikipanga shughuli zake kivyake, lakini sasa wamekuwa wakishirikiana kwa karibu. “Mfano, kwa sasa Afisa Lishe anashiriki nasi kutushauri kuhusu chakula tunachotoa mashuleni ili kiwe na virutubisho. Hata zinapokuja masuala ya malezi na makuzi katika shule zetu, tumekuwa tukishirikiana kuyatatua,” alisema.



0 Comments