AZIZA MWANAMKE MUOKOTA MAKOPO ALIYEFANIKIWA KIUCHUMI


 Na Asha Mwakyonde

DHAHABU ili ing'ae lazima ipite kwenye moto, Usemi huu naufafanisha na jitihada na mafanikio ya Aziza Abdallah mwanamke ambaye alipitia changamoto nyingi hadi kufanikiwa katika safari yake ya kuokota chupa za maji kwa lengo la kujipatia kipato.

Aziza aliacha kazi ya ushonaji nguo na kujiingiza katika kuokota chupa kwenye jalala (Dampo),huku marafiki zake wakubwa  wakiwa ni wa watoto wanaishi katika mazingira magumu (Watoto wa mitaani) Kwa kipindi cha miaka sita.

Kwa sasa Aziza na mume wake wanamiliki kiwanda cha kusaga chupa kiitwacho Cal plastc recycling ambacho kinamilikiwa na familia yao.

SAFARI YA MAFANIKIO YAKE

Aziza amesema kuwa  biashara hiyo ya kuokota chupa aliianzia  Dar es salaam baadaa ya kuelezewa matumizi ya chupa ambazo zimetumika ndipo alivyorudi Dodoma na kuanza rasmi kuingia dampo.

"Sikuwa na mtaji wala fedha kwa ajili ya kununulia chupa, niilianza kuokota makopo mwenyewe kwenye matololi ya nataka na  najaza kwenye neti na kuyafunga, mume wangu anachukua na kuyapeleka Dar es salaam kuuza na kuleta kipato," amesema Aziza.

Ameongeza kuwa baada ya miaka mitatu waliona kazi ni ngumu kontena kubwa la fourt feety  linapakia kilo1300 ambazo ni kidogo huku akisema kuwa fedha nyingi walikuwa wakimpatia dereva.

"Unakodi gari laki tano unampa dereva akienda kuuza faida inakuwa ni laki moja nikafikiria ni mbinu gani ili hii laki tano ya dereva ibaki kwangu nikaenda kuomba mashine kwa mhindi nikaambiwa nilipie asilimia 50 wakati huo ilikuwa inauzwa milioni 15, mwaka 2003 milioni 15 ilikuwa ni fedha nyingi sana hasa kwa mtu ambaye hajawahi kuishika," amesema Aziza.

Amefafanua kwamba alifanya maamuzi magumu kwenye familia yake ya kuuza kiwanja ambacho kilikuwa tayari kilishaanza kujengwe (Pagale), wakanunua mashine hiyo huku wakiendelea kupanga chumba kimoja wakati huo wakiwa na mtoto mmoja Pamoja na ujauzito.

Kwa mujibu wa Aziza baada ya kununua mashine hiyo wakawa na changamoto sehemu ya kuiweka ambapo walirudi tena kwa mhindi kuomba kukopeshwa fedha kiasi cha shilingi milioni tatu ambazo zilitumika kukodi gadauni na kufunga mashine na kuanza kusaga chupa hizo.

Amesema wakisaga kontena la fourt feety wanapakia tani 24 kwa gharama ile ile ya laki tano ambayo awali walikuwa wakilipa kwa tani moja na nusu huku akisema kuwa ndio mwanzo wao  ulipoanzia wa kupata faida.

"Tukaanza kutengeneza ajira, tukaanza kupata maendeleo tunamshukuru Mungu kuanzia hapo mwaka 2003 hadi 2023 tumepiga hatua kubwa sana, naamini kila mtu akitumia fursa kwa kutumia akili yake mwenyewe anaweza kufanikiwa, leo hii najulikana natambulika napewa mikopo ni kwakuwa nilijituma zaidi," ameongeza.

"Kiwanda chetu Cal plastc recycling kinamilikiwa na familia, nimefurahi kuwaona na kutembelewa na wageni kama nyie waandishi wa habari ndio mnaopeleka habari kwa wananchi, tuna changamoto ya ajira naamini watakaopata taarifa hii wengi watajua chupa ni ajira tuna kaulimbiu tuna sema "Kuokota chupa,makopo sio laana ni ajira" amesema Aziza.

Amesema kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 46 kwa kazi mbalimbali zikiwamo za kuokota chupa, kuzichambua huku akieleza kuwa ana viwanda vingine Nzuguni jijini  hapa na Dar es salaam hivyo wapo wafanyakazi wengine.

Ameeleza kuwa viwanda hivyo vinatumika kusaga chupa katika hatua ya kwanza kwa ajili ya kupata urahisi wa kusafirisha.


MAFANIKIO YAKE

Aziza amesema kuwa wakati anaza hakuwa na gari bali alikuwa na baiskeli ambayo waliokuwa wakipakizana na mume wake kwenda dampo kuokota chupa na kwa sasa wanamiliki gari za kutembela kila mtu na lake.

"Nilianza nikiwa nakaa chumba kimoja kwa sasa nina zaidi ya nyumba nne zote ni nzuri nyingine zinawapangaji kingine ninachojivunia nina gari aina ya kenta mbili, Skania moja, semitela moja nilipofika nimepiga hatua kubwa sana," amesema Aziza.

KUHUSU SOKO

Aziza amesema awali Tanzania haikuwa na kiwanda cha kutengeneza nyuzi aina ya polyester ambayo inatumika kutengenezea nguo hivyo walikuwa wakisaga chupa hizo na kupeleka China na kwamba kwa sasa kuna kiwanda hicho Mlandizi mkoani Pwani cha Wachina.

" Nyuzi hizi aina ya polyester ndio zenye soko ambazo zinatokana na mabaki ya petroli  hivyo petroli ikipanda na chupa zinapanda kwa kuwa malighafi zinatumika kwa wingi zaidi na soko linakuwa ni kubwa. Petroli ikishuka na chupa zinashuka bei wanaona ni bora wachukue uchafu unaotokana na mafuta haya kuliko kununua chupa," amesema.

Amefafanua kuwa awali  baada ya kusaga chupa hizo walikuwa wanapeleka china kutokana na Tanzania kutokuwa na kiwanda cha kuyeyusha chupa hizo na kupata nyuzi aina ya polyester.

CHANGAMOTO 

Amefafanua kuwa katika biashara hiyo changamoto zipo lakini kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita petroli  imepanda hivyo hawana changamoto ya soko.

Aziza amesema kuwa changamoto ya soko inatokana na mafuta ya pretroli inaposhuka bei kwa wafanyabiashara huyo wanapata hasara.

"Lakini kwa bahati nzuri ninafanya biashara na Waturuki Nina mkataba na Waturuki sina mkataba na Wachina  mwaka jana Septemba kulikuwa na changamoto ya soko na  kwamba mzigo wake anausafirisha moja kwa moja kwenda Uturuki.

Aziza amesema tetemeko  la Uturuki ambalo limetokea mwaka huu Februari liliwaathiri na kwamba hawakulipwa hela zao ambapo hadi sasa wanadai zaidi ya milioni 200.

"Hivi karibuni nilienda Wizara ya Viwanda na Biashara na kuelezea changamoto iliyotokea kwa sababu wale ni wawekezaji wapo Kisheria na nimewekeza kwao. Wizara ilinipatia ushirikiano wa kutosha iliwasiliana na kufanya mazungumzo nikaabiwa nivute subra kwa kuwa kiwanda chao chote kimebomoka na wamepata hasara kubwa," amesema.

"Hata wakati nauza kiwanja, nyumba iliyofikia kwenye renta ndugu walikutana wakasema namdanganya mume wangu lakini hawadhani kama biashara ya chupa inaweza kunisaidia ila nilijitahudi kumshawishi mume wangu hadi akanielewa nilimwambia familia ni mimi na wewe hao wengine watasema tu," amesema.

Akizungumzia waonaookota chupa na kuiba vitu vya watu wanapopita kwenye nyumba za watu amesema wengi wanafanya hivyo kutokana na maisha magumu huku akisema wenye tabia hiyo kwa sasa wamepungua kutokana na elimu anayowapatia.

KUHUSU ELIMU

Akizungumzia elimu yake ameeleza kuwa sio msomi elimu yake ni ya kawaida ya kidato cha nne aliyoipata kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1992 katika shule ya sekondari Jumuiya iliyopo mkoani Tanga.

Mmiliki huyo amesema kuwa awali baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari alikuwa fundi nguo na alikuwa akiwashonea viongozi mbalimbali wakiwamo Mawaziri.


MTAZAMO WA JAMII

"Wakati naanza kuokota makopo jamii iliniona ni mtu wa ajabu, mimi ni mzaliwa wa Tanga dada yangu ni kiongozi watu walimfuata na kumwambia mdogo wako ameamua kushinda jalalani ( Dampo), umeshindwa kumsaidia?. Dada yangu aliniita nilimwambia kwenye maisha lazima nipambane nina familia yangu ya mtoto mmoja nahitaji niwe na familia kubwa niwe na maisha mazuri, sihitaji maisha ninayoyapitia apitie mtoto wangu,"amesema.

Amesema kuwa hata mume wake hakukuliana naye kuokota chupa  kutokana na kufahamika mkoani hapa kwa kazi yake ya ushonaji nguo ambapo aliwashonea Mawaziri na kwamba  wengi walidhani ni kichaa cha ujauzito.

Aziza ameongeza kutokana na changamoto za maisha alijitoa ufahanu akaingi dampo kuungana na watoto wa mitaani kuokota chupa hizo na kwamba watoto hao wanamfahamu vizuri aliishi nao zaidi ya miaka sita.

WITO WAKE KWA WANAWAKE

Amewataka kutokukaa nyumbani  kusubiri fursa iwafuate na kwamba hawataipata bali waitafute na wakianzisha kitu wakisimamie watafanikiwa.

Ameeleza kuwa akina mama wanaweza na mwanamke akisema hana ajira sio kweli bali hajataka kutafuta ajira zipo na ni kwa namna anavyoweza kuitafuta fursa.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI