TASAC: TANZANIA NA UGANDA KUTEKELEZA MRADI WA BILIONI 59.23


 Na Asha Mwakyonde Dodoma 

SERIKALI ya Awamu ya Sita kupitia
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) inaendelea kukamilisha Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport MLVMCT).

Mradi huu unaotekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda umepangwa kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 59.23 ambapo upande wa Tanzania gharama za mradi ni Shilingi Bilioni 19.97 zinazojumuisha gharama za kazi za ndani na sehemu ya mchango wa Tanzania katika kugharamia kazi za kikanda zinazofanywa kwa kushirikiana na Uganda. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mnano mwezi Desemba, 2024 na tayari Mshauri Elekezi ameshakabidhiwa maeneo ya kufanyia kazi. 

Akizungumza Jijini Dodoma Machi 7,2023 kuhusu utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo pamoja na mafanikio katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Kaimu Mkeyenge amesema lengo la mradi huo pamoja na mambo mengine ni kujenga vituo vinne vya uokozi (search and rescue centres-(SARs)) ambavyo vitakuwa kimoja kimoja katika maeneo ya Kanyala Sengerema, Musoma - Mara, Nansio - Ukerewe na Ilemela Mwanza.

Mkurugenzi huyo ameeleza vituo hivyo  vitasaidia katika kushughulikia changamoto za usafiri kwa njia maji na katika uokozi majini, kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri kwa njia maji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria. 

Mkeyenge ameongeza kuwa uendelezaji na Uimarishaji wa Miundombinu ya Mifumo ya TEHAMA TASAC inatekeleza miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika kuhakikisha manunuzi, matumizi bora, sahihi na salama ya vifaa na mifumo yote ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini.

"Katika kutekeleza hili, Shirika limeunganisha ofisi zake zote zikiwemo zile za Mikoa, Wilaya na mipaka kwenye Mkongo wa Taifa ambao umerahisisha na kuharakisha mawasiliano ya ndani (Intranet), barua pepe, na mawasiliano na wadau wa nje (Internet)," amesema
Mkeyenge.

Aidha amefafanua kuwa  uendelezaji miundombinu na mifumo ya TEHAMA ulianza mwaka wa fedha 2018/19 na utakamilika mwaka wa fedha 2025/26.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa Miundombinu na mifumo ya TEHAMA inayoboreshwa ndani ya Shirika ni pamoja na mfumo wa ukaguzi, usajili wa vyombo vya usafiri kwa njia ya maji na utoaji wa vyeti vya Mabaharia (Maritime Administration Management System), mfumo wa utoaji leseni, ukusanyaji wa mapato ya udhibiti, uhakiki kadhia na kutoa ankara za malipo ya watoa huduma wa meli (Manifest Billing System), pamoja na mfumo wa kutoa huduma za biashara ya Meli (Shipping Business Management System SBMS).

Pia Mkurugenzi huyo ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu H kwa kuendelea kuiwezesha na kuisaidia TASAC ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

"Naishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi chini ya Waziri wetu Prof. Makame Mbarawa, kwa kuendelea kutusimamia na kutuongoza vyema katika utekelezaji wa majukumu yetu," amesema Mkeyenge.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI