Mmoja wa Maafisa gereza la Bukoba akipokea bango la uelimishaji kuhusu ugonjwa wa Marburg.
Na Elimu ya Afya kwa Umma.
JUMLA ya watu 805 wakiwemo wafungwa, watumishi wa magereza pamoja na familia zao katika Gereza la Bukoba Mkoani Kagera wamefikiwa na elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa Marburg .
Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Dkt.Tumaini Haonga baada ya kutembelea gerezani hapo kutoa elimu namna ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg, Beauty Mwambebule amesema Marburg ni muhimu kuchukua tahadhari mapema juu ya ugonjwa huo.
“Kinga ni bora kuliko tiba ; wakati mwingine inaweza kuchukua kuanzia siku 2 hadi 21 kuonesha dalili mfano homa, kutapika, kuharisha damu au kutapika damu ni muhimu tuchukue tahadhari mapema” amesema Beauty Mwambebule, Mwakilishi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya.
Kwa upande wake Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Jackline Saulo amesema ni muhimu kwa kila mtu kuepuka misongamano isiyo ya lazima ambapo pia maelekezo yameshatolewa kuhakikisha sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu panakuwepo na vifaa maalum vya kunawia mikono.
Wakitoa neno la shukrani baadhi ya watumishi wa Gereza la Bukoba akiwemo Mkaguzi wa Jeshi la Magereza Fredrck Katabazi huku Mkaguzi Msaidizi Venance Vedastus ambaye ni afisa mapokezi gereza la Bukoba wametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mara tu yanaporipotiwa hasa kwa kuongeza wigo wa uelimishaji.
Pia katika gereza la Bukoba yametolewa mabango yenye ujumbe mahsusi kuhusu elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa Marburg , dalili zake na jinsi unavyoenezwa.
Ikumbuke kuwa watalaam wa Afya kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera wameendelea kutoa elimu jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera kwa kufikia makundi mbalimbali ikiwemo magereza, viongozi wa dini, waendesha pikipiki, maduka na sehemu zote za kutolea huduma na sehemu zenye mikusanyiko.
0 Comments