FAHAMU ALICHOKISEMA BABA WA MTOTO WA SIKU 27 ALIYEFANYIWA UPASUAJI JKCI


 Na Asha Mwakyonde

"KWA wale wenye watoto ambao wanatatizo wasiamini kuwa ni tatizo la 
kudumu, mtoto wangu amepona na hana tatizo la moyo tena na nikimpeleka kuhudhuria kiliniki wataalam wanasema hana shida yoyote na anacheza vizuri" haya ni maneno ya mkazi wa Arusha Elibariki Shoo katika maojiano maalumu na mwandishi wa makala haya.

Shoo pia ameishauri Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI),kuhamishia wataalam wake katika  kila Mkoa ili iwe rahisi kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo kutokana na watoto wengi kuwa na tatizo hilo  na kushindwa kugundulika mapema.

Akizungumza  hivi karibuni katika maadhimisho ya miaka 70 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga yaliyofanyika mkoani Dodoma, amesema  huduma hiyo ikiwepo kila Mkoa wazazi watakuwa wakitembelea mara kwa mara na kubaini watoto wao kwa haraka endapo watakuwa na tatizo hilo.

Shoo amesema kuwa mtoto wake  alipata changamoto ya kuugua ugonjwa mfumo ya  mishipa mikubwa miwili ya moyo kubadilishana katika sehemu inayoanzia 'Transposition of great arteries (TGA)' Oktoba mwaka 2019.

Amesema kuwa mtoto wake alizaliwa akiwa na afya njema lakini baada ya siku saba alianza kupata shida ya kushindwa kunyonya, kupumua ambapo walimpeleka  Hospitali ya Mount Meru na kufanyiwa vipimo aligundulika ana  shida katika mfumo wa moyo ambapo walipewa rufaa ya kwenda katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Mkazi huyo wa Arusha ameeleza kuwa baada ya kufika JKCI mtoto huyo alionekana anashida hiyo ya mfumo wa kupeleka damu kwenye moyo ambao ulikaa upande kushoto na wa kushoto ulikaa upande wa kulia.

Amesema ilikuwa ni changamoto kwa kuwa mtoto huyo alikuwa na umri mdogo wa siku 27 na kwamba alifanyiwa upasuaji  ambao alitakiwa kumpeleka  mtoto huyo nje ya nchi kupatiwa matibabu.

"Ilikuwa ni upasuaji wa kwanza katika taasisi hiyo  wa TGA ambapo alifanyiwa oparesheni tatu. Upasuaji wa kwanza  ni kumsaidia kunyonya wa  pili ni kubadilisha mishipa iliyopishana na ya tatu ni wa kumsaidia kupumua  baada ya upasuaji tulikaa miezi mitatu katika taasisi hii," amesema Shoo.

Ameongeza kuwa upasuaji huo ulifanywa na madaktari bingwa  mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwamo kutoka Sweden na mtoto huyo aliendelea vizuri hadi sasa ana umri wa miaka mitatu na nusu.

Pia amewapongeza wataalam wa ndani na nje ya nchi walioshirikiana kufanya upasuaji wa mtoto huyo huku akiipongeza taasisi ya JKCI pamoja na kitengo cha Ustawi wa jamii kwa kuwezesha mtoto wake kupata huduma.

"Mtoto wangu anaendelea vizuri na anahudhuria kiliniki kila mwaka. Namshukuru Mungu huduma hii imetusaidia hasa kwa sisi Watanzania ambao ni wa hali ya kawaida," ameeleza Shoo.

GHARAMA ZA MATIBABU

Akizungumzia gharama za matibabu kwenda nchini India  amesema kuwa aliambiwa zaidi ya milioni 30 na ilikuwa ni changamoto kwake ambapo alianza kuomba msaada kwa kuwachangisha ndugu, jamaa na marafiki zake.

Shayo amesema kuwa katika taasisi ya JKCI upasuaji wa kwanza uligharimu milioni 4.4  na wa pili uligharimu milioni 8.8 ambapo walipata punguzo la nusu  gharama kila upasuaji kutoka kitengo cha Ustawi wa jamii kilichopo katika taasisi hiyo.

WITO WAKE KWA JAMII

Amewataka wanajamii kuwa na utaratibu wa kwenda Hospitali bila kujali wanafedha au laa kwani wanaweza kusaidiwa kupata matibabu kama alivyosaidiwa.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA