WAANDISHI WA HABARI WAPATIWA MBINU ZA KUTAMBUA HABARI PICHA,VIDEO ZISIZO ZA KWELI


Mkuu wa kitengo cha Mafunzo kutoka Nukta Africa Daniel Mwingira akifafanua jambo kwa waandishi walioshiriki mafunzo ya Fact checking.

Na Asha Mwakyonde, aliyekuwa Arusha

WAANDISHI wa habari zaidi ya 30, kutoka mikoa mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo 'Fact checking' ya kutambua habari  zisizo za kweli kupitia njia za mitandao ya 'Google image,Tin Eye na RevEye kwa lengo la kuthibitisha habari ambazo wanazitilia shaka kabla ya kupelekea Umma.

Mafunzo hayo yametolewa na Shirika Huru lisilo la faida la Africa Check  kwa kushirikiana na kamapuni ya Habari na Teknolojia ya Nukta Africa yenye lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari kubaini habari picha,video zikiwamo za viongozi mtandaoni zisizo za kweli ili kuepuka kuzitumia.

Akizungumza hivi karibuni jijini Arusha  wakati wa mafunzo ya siku mbili Mkufunzi kutoka shirika la Africa Check ambaye pia ni Mhariri wa shirika hilo  nchini Kenya Alphonce Shiundu  amesema kuwa duniani kote kila mwandishi anapoandaa habari ni lazima afuate msingi wa habari zenye uhakika ambazo wanahabarisha Umma ili kuepuka taharuki.

"Waandishi hawa wamepatiwa mafunzo haya na njia watakazotumia ili kuhakiki habari picha na video zisizo za kweli na ambazo wanazitilia shaka  na njia hizo zitawasaidia katika kazi zao," ameeleza Shiundu.

Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka shirika la Africa Check, Makinia Juma amesema kuwa njia ambazo mwandishi anazoweza kuzitumia katika kuhakiki habari picha na video feki ni kwa kutumia 'Google image, TinEye na RevEye ili kuthibitisha habari zao.

"Endapo mtatumia njia hizi vizuri mtaepuka kuandika habari picha na video zisizo za kweli na badala yake umtahakiki  na kuandika zenye ubora," amesema Makinia.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Mafunzo kutoka Nukta Africa Daniel Mwingira ameeleza kuwa waandishi hao watabadilisha aina ya uandishi wao kupitia njia walizofundishwa.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari ambapo  dunia ya sasa inaenda kasi kutokana na Teknolojia  hivyo ni vema wakazingatia njia hizo.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Highlands Fm Radio Mbeya, Frances Mwakibete amesema kuwa mafunzo yalikuwa mazuri  yamemjengea uwezo na mbinu za kujua na kutambua habari za kweli na zisizo za kweli.

"Mifumo ya ufundishaji ilinifanya niweze kuelewa darasa vizuri mno, mimi kama mwandishi haitanisumbua katika  kuthibitisha habari kama ni za kweli au za uzushi," amesema Mwakibete.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA