Baadhi ya Watumishi wa BRELA , wakiwa katika picha ya pamoja na watoto wanaolelewa katika Kituo cha Watoto Yatima AL-Zam Orphanage Center, kilichopo Mbagala Jijini Dar es Salaam.
Dar es salaam
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa msaada wa bidhaa mbalimbali za chakula pamoja na mahitaji mengine katika kituo cha watoto yatima kinachojulikana kwa jina la AL-Zam Orphanage Center kilichopo Mbagala Zakhiem Wilayani Temeke, Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya mahitaji yaliyotolewa ni pamoja na mafuta ya kupikia, ,sukari, unga wa sembe, mchele, maharage, nyama, sabuni, madaftari, dawa ya meno, miswaki, pipi, na kalamu.
Afisa Leseni kutoka BRELA Bw.Koyan Abubakar akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa ameeleza kuwa lengo kubwa ni kuwatia moyo watoto na uongozi wa kituo hicho kwa kazi kubwa wanayoifanya ili kuongeza juhudi ya kuwahudumia wahitaji ili kufikia ndoto zao.
“BRELA ni Taasisi inayosimamia Sajili za kibiashara na Leseni, imefika katika kituo hiki kwakuwa ni sehemu ya jukumu la Taasisi la kurejesha kwa jamii mbali na majumu ya msingi ya Taasisi", amesema Bw. Koyan.
Kwa upande wake Afisa Msajili Mwandamizi, Bw. Lugano Mwampeta amewaeleza watoto wanaolelewa katika kituo hicho baada ya kueleza ndoto zao katika moja ya nyimbo walizoimba kuwa, njia kuu ya kuzifikia ndoto zao ni kwa kufuata mafundisho wanayopatiwa na walezi wao kituoni hapo.
“Njia kuu ya kufikia ndoto zenu ni kufuata mafundisho mnayopatiwa na walezi hapa kituoni, pia ili muweze kufikia ndoto hizo ni kufanya bidii katika masomo shuleni”, amefafanua Bw. Mwampeta.
Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Zainab Said Buleta, ameishukuru BRELA kwa msaada huo ambao utawawezesha watoto hao kujikimu.
Bibi Zainab ameongeza kuwa, kituo hicho kilianza kwa kuwalea watoto 10 lakini hivi sasa kinalea watoto 60 kati ya hao 35 ni wasichana na 25 ni wavulana.
0 Comments