NZOWA AIPONGEZA SERIKALI YA RAIS DK. SAMIA KWA KUVIJALI VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI

 

Mkuu wa chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kisangwa (FDC), Edmund Nzowa akitoa  maelezo kuhusu Chuo hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule alipotembelea katika banda hilo kwenye maonesho ya wiki ya Ubunifu Kitaifa (IWTZ),yenye kauli mbinu isemayo ' Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kuchangia Uchumi wa Bluu.

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

WANANCHI wametakiwa kuthamini mafunzo ya ufundi stadi kwa kuwa ndio mafunzo pekee yanayofungua fursa za ajira za moja kwa moja kwa vijana  bila kusubiri kuajiriwa na serikali, taasisi au kampuni.

Pia Serikali imeombwa  kuajiri watumishi katika  Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC),kutokana na Vyuo hivyo kukabiliwa na uhaba wa watumishi hao ili kutosheleza idadi.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma Aprili 25, 2023 na Mkuu wa chuo Cha maendeleo ya Wananchi Kisangwa (FDC), Edmund Nzowa katika banda la Vyuo hivyo kwenye maonesho ya wiki ya Ubunifu Kitaifa  (IWTZ),yenye kauli mbinu isemayo ' Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kuchangia Uchumi wa Bluu.

Nzowa amesema  Vyuo hivyo vinawaandaa vijana ili waweze kuingia katika soko la ajira na kwamba vinamchango mkubwa kwa vijana ambapo wanaiomba serikali kuwaongezea watumishi.

Ameeleza kuwa mwanafunzi anaposoma katika Vyuo hivyo anapata ajira moja kwa moja bila kutegemea ile ya kuajiriwa kwa kuwa tayari anakuwa na ujuzi wake.



"Banda hili kama mnavyoliona linafanya shughuli za maendeleo ya wananchi, katika Vyuo vya wananchi kuna program mbili ambazo tunazifanya," ameeleza .

Amefafanua kuwa program hizo ni za  ufundi stadi ambazo zinahusisha masomo ya fundi mbalimbali na program ya Elimu Haina Mwisho ambayo inawasaidia watoto waliokatisha masomo yao kutokana na sababu za kijamii ikiwamo kupata ujauzito katika umri mdogo.

Nzowa ameongeza kuwa kuna dhana, vifaa mbalimbali vya mafunzo ambavyo vinatengenezwa kwenye Vyuo vya maendeleo ya wananchi lengo likiwa ni kusaidia katika ufundishaji na ufundishwaji kwa wanafunzi ambapo vinasaidia katika ufundishaji.

Mkuu huyo wa Chuo amesema baada ya kuona kuna changamoto ya vifaa vya ufundishaji walianza kutengeneza ili kuepuka gharama za kununua nje ya nchi na kwamba vifaa hivyo au dhana za ufundishaji zimekuwa ni mchango mkubwa kwa wanafunzi kutokana na mafunzo wanayoyatoa ya ufundi.


"Kwa kutumia dhana hizi, vifaa wanafunzi wanapomaliza wanakuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa  umahiri katika ufundi wao. Elimu ya sasa tunahitaji vijana wanapomaliza  wawe mafundi mahiri katika soko la ushindani, tunaimani vifaa wanavyotumia kujifunza na wanapomaliza tunatoa mazao ya uhakika wa kuuzika katika ajira, kujiajiri  wenyewe," amesema Nzowa.

Akizungumzia Elimu Haina Mwisho Mkuu huyo amesema kuwa wao ni moja ya taasisi ambayo inatoa elimu ya kuwasaidia waliokatisha masomo na kwamba kauli ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wanamuunga mkono ambapo kwa sasa wanaidadi kubwa ya watoto wanaopata elimu kwa mfumo usio rasmi.

CHANGAMOTO

Mkuu huyo ameeleza kuwa mbali na  changamoto ya watumishi katika Vyuo hivyo vya Maendeleo ya wananchi wanachangamoto nyingine  ambayo ni ya  vifaa na kwamba kutokana na Teknolojia inavyobadilika wanahitaji vifaa zaidi vya kufundishia.


Nzowa ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dk. Samia ambapo amevijali Vyuo vya ufundi stadi vikiwamo Vyuo vya maendeleo ya wananchi kwa kupeleka vifaa vya mafunzo katika Vyuo hivyo na kuvikarabati.

Ameongeza kuwa kuna Vyuo 54 vya maendeleo ya wananchi ambavyo vilianzishwa mwaka 1975.

Awali Mkuu wa Mkoa Dodoma Rosemary Senyamule  alipotembelea banda la Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi  amewapongeza  kwa ubunifu wa kutengeneza dhana za kufundishia ambazo vimekuwa zikileta matokeo mazuri kwa kuzalisha vijana wenye uwezo mkubwa wa kujiajiri wenyewe.


Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU