PROF. RUGGAJO: MADHARA YA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU NI MAKUBWA, WANAWAKE WALIOKOMA HEDHI WAPO HATARINI


 Na Asha Mwakyonde 

SHINIKIZO la juu la damu (Hypertention), ni ugonjwa unaosababishwa na nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa kuwa mikubwa kuliko kawaida kwa muda mrefu.

Kuna aina mbili za ugonjwa huo ambazo ni Shinikizo la juu la damu asili (Primary Hypertention), na Shinikizo la juu la damu linalosababishwa na magonjwa mengine ( secondary Hypertension.

Kadri ya asilimia 90 hadi 95 za watu wanaoathiriwa na ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu la asili  waliugua ugonjwa huo bila kuwa  na chanzo cha kisayansi kinchofahamika.

Shinikizo la juu la damu linalosababishwa na magonjwa mengine (secondary Hypertension),hutokana na magonjwa ya figo,mapafu, mfumo wa homoni ambao huathiri asilimia 5 hado 10 iliyobaki ya watu wenye Shinikizo la juu la damu.

Akizungumzia ugonjwa huo Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Profesa Paschal Ruggajo amesema Shinikizo la juu la damu huchangia asilimia 12 ya vifo ambayo vinatokana na magonjwa yasiyoyakuambukiza hospitalini.

Prof. Ruggajo ameeleza Shinikizo la juu la damu ni kubwa na linapanda chini ya ukanda wa Jangwa la Sahara katika nchi na takwimu kwa kipindi cha miaka mitano limeongezeka mara mbili zaidi ndani ya muda mfupi.

"Tunasisitiza kupima kwa usahihi kuna mchakato wa namna ya kupima Shinikizo la juu la damu ambao unatumika kufuatilia ili kutoa namba ambayo ni sahihi. Tunaendelea kutoa wito kwa watoa huduma wetu wazingatie yale maelekezo ya kumpa mgonjwa kabla ya kumpima," amesema Prof. Ruggajo.

Akifafanua kuwa mgonjwa anatakiwa kuwa amekaa kwenye kiti ametulia kwa zaidi ya dakika tano kabla ya kuanza kupima, asiwe amevuta sigara, kunywa kahawa, atulie kwenye kiti na mkono uwe usawa wa moyo.

Prof. Ruggajo amesema katika mazingira ya kutokupima kwa usahihi kuna hatari ya kutoa namba ambayo sio sahihi na kwamba wastani wa kupima Shinikizo la juu la damu ni mara tatu na baada ya hapo vipimo vitakavyofuata na dawa vitaendana na ugonjwa kama upo.

MADHARA YAKE

Prof. Ruggajo ameeleza kuwa mtu  mwenye ugonjwa huo anakuwa yupo kwenye hatari ya kupata kihausi 'Stroke', kuugua kwa mishipa midogo ya damu, kupunguza uoni na kusababisha upofu,
 huongeza  nafasi ya moyo kupata shambulio la ghafla  la moyo na pia moyo kujaa misuli kwa sababu ya kujaribu kusukuma damu kwa mahitaji yale yale ya miwili wakati Shinikizo la juu la damu linakuwa limezidi kwenye mishipa.

Ameongeza kuwa viungo kama figo huathirika moja kwa moja kwa shinikizo la juu la damu lililopanda.

"Wote tuna fahamu matibabu tanayotokana na ugonjwa wa figo yalivyo ambavyo yanaathiri kwenye pato la mtu mmoja mmoja la familia na la Taifa, haya yote ni madhara makubwa ambayo yanagharimu  kiasi kikubwa cha fedha katika kutibu," amesema.

KUHUSU UPIMAJI

Akizungumzia kuhusu upimaji wa Shinikizo la juu la damu Prof. Ruggajo ameeleza kuwa wananchi wenye umri  chini ya miaka 40  wanashauriwa kupima angalau mara moja au mbili kwa mwezi ili kufahamu namba zao za kiwango cha ugonjwa huo.

"Watu wenye umri wa miaka 40 hadi 60 wanashauriwa kupima mara nne kwa mwezi na wale ambao umri zaidi ya 60 nao wanashauriwa kupima mara mbili kwa wiki, hawa tunawazungumzia wale ambao wapo kwenye jamii na hawajui ugonjwa huu kutokana na kupima ndo watagundua," amesema.

Prof. Ruggajo amefafanua kuwa kwa wale ambao wameshagundulika na  wapo kwenye matibabu ya dawa wanatakiwa wapeme mara tatu kwa wiki huku akiwasiaitiza kuzingatia masharti ya madaktari wao wanaowatibu  ikiwa ni pamoja na kutumia dawa hizo kwa kadri zilizopangwa na kuepuka vitu vingine vinavyoweza kusababisha au kuchochoe Shinikizo la juu la damu lisiweze kudhibitiwa.

"Vichochezi ni vingi kwa bahati mbaya sisi Waafrika imeonekana tuna asili ya kupata Shinikizo la juu la damu zaidi kuliko wenzetu wa mabara mengine,
madhara ya chumvi kwenye miili ya Waafrika ni makubwa zaidi kuliko mabara mengine.

VINASABA

Prof.Ruggajo amefafanua kwamba vinasaba  pia kwenye shinikizo la juu la damu likiwepo katika familia fulani wale wanaozaliwa kwenye familia hizo wananafasi kubwa zaidi ya kuwa na ongezeko kuliko wengine ambao hawajazaliwa kwenye familia hizo.

Aidha Prof.Ruggajo ametoa wito kwa wale ambao labda baba,mama, mjomba shangazi wana ugonjwa huo ni vizuri kupima mara kwa mara na wawe wanakumbuka uwezekano wa wao kupata shinikizo la juu la damu ni mkubwa kuliko mtu mwingine yoyote.

AKINA MAMA AMBOA WAMEKOMA HEDHI

Prof. Ruggajo amesema akina mama ambao wamekoma hedhi uwezekano wa kupata ugonjwa huo ni mkubwa kuliko miaka ambayo walikuwa bado wanahedhi zao.

Mkurugenzi huyo ameshauri kupunguza matumizi ya chumvi kwa kuwa inashupaza mishipa ya damu inasababisha damu inashindwa kupita kwa urahisi kwenda katika viungo vya mwisho kwa sababu  ndio inayopelewa hewa Safi ya Oksjeni na chakula.

"Kadri damu inavyoshindwa kupita kwa sababu ya mishipa kushupaa ile presha inarudi kinyume nyume hadi kwenye moyo na inautanua na baadae inajaza misuli kwenye moyo na kusababisha ugonjwa huu,"amesema.

Ameongeza kuwa kitaalam chumvi inatakiwa kutumika chini ya gramu mbili kwa siku, kijiko kidogo cha chai kikiwekwa msawazo huku akisema matumizi hayo yanatakiwa kupungzwa kadri umri unavyozidi kuwa mkubwa.

"Tunashauriwa kupunguza mafuta ya kula hasa  yatokanayo na asili ya wanyama  tunashauriwa kutumia ya mimea zaidi kwa kiasi kidogo yakiwamo alizeti, pia tule chakula ambacho kina mlingano mzuri,ameeleza Prof. Ruggajo.

Amefafanua kuwa nusu ya sahani ya mviringo inatakiwa kuwa na matunda pamoja na mboga za majani, nusu nyingine igawanywe mara mbili robo iwe na chakula cha protini kama vile dagaa, samaki, nyama na robo ngingine chakula cha wanga ili kumpatia mtu nguvu za kufanya kazi.

Prof. Ruggajo amesema wanga unaoshariwa ni ule ambao haujakobolewa ambao una nyuzi nyuzi  kama vile mtama, magimbi, mihogo, viazi, vyakula vya asili  vinavyokuwa na wanga vinaenda kutoa sukari kidogo kidogo mwilini ni chakula bora ambacho kitasaidia kupunguza Shinikizo la juu la damu.

"Tunaendelea kusisitiza unadhibiti uzito wako na kuhakikisha pia kwenye suala la uzito kuweza kudhibiti  uwiano ulipo kati ya uzito na urefu wako wa mwili,pia tafiti zinaonesha uzito ambao umeongezeka maeneo ya tumboni,kiriba tumbo na kitambi hivyo vyote ni vichochezi vikiongezeka vinaenda kusababisha ugonjwa huu," ameeleza Prof.Ruggajo.

AFYA YA AKILI

Akizungumzia afya ya akili Prof. Ruggajo amefafanua kuwa kitu kingine ambacho kinasababisha ugonjwa wa shinikizo  la juu la damu ni afya ya akili hivyo kupunguza msongo wa mawazo,kupumzika, kufanya mazoezi ni moja ya kumpunguzia mtu msongo wa mawazo.

"Mazoezi mazuri ni yale yanayohusisha misuli mingi ya mwili kama vile kutembea kwa kasi, kukimbia, kuendesha baiskeli na kuongelea, tunashawishi sana mtu kujiwekea programu yako ya kuwa na lishe bora, mazoezi pamoja na mapumziko hivi vitu vinachangia nafasi ya kupata Shinikizo la juu la damu," ameeleza.

SERIKALI

Prof. Ruggajo amesema serikali inaendelea kuwekeza katika vifaa tiba, miundombinu na watumishi pamoja na kuendelea kupeleka ugunduzi mapema kwenye matibabu ya ugonjwa huo katika afya ya msingi kwenye zahanati na vituo vya afya.

Ameongeza kuwa kwa kiasi kikubwa serikali imejitahidi kuwekeza kwenye Hospitali za mikoa, Kanda, Rufaa na Hospitali maalumu huku akisema wananchi wengi bado wanatafuta huduma katika afya ya msingi.

Prof. Ruggajo amesema kwa kushirikiana na wadau wamesambaza vifaa tiba, wamefanya mafunzo na kwamba serikali baada ya kugundua wananchi wengi wanatibiwa kijijini na matibabu ya Shinikizo la juu la damu yanatakiwa yaanzie kule ili kuepuka matatizo.

Amesema serikali mwaka huu imeamua kupeleka dawa za kupunguza ugonjwa huo kwenye afya ya msingi huku akisema dawa tatu ambazo zimeshushwa kutoka Hospitali ngazi ya Wilaya, Halmashauri kwenda ngazi ya kituo cha afya ni Losartan,Amlodipine na  Hydralazine.

"Dawa hizi zimeshushwa kutoka hospitali ya Wilaya zinakwenda katika hospitatli ngazi ya kituo cha afya hivyo hivyo kuna dawa mbili ambazo zimetoka ngazi ya kituo cha afya kwenda ngazi ya zahanati ambazo ni Nifedipine  na Furosemide, serikali imechukua hatua za makusudi na kuweza kupunguza uwezekano wa kupata madhara ya kukaa muda mrefu mgonjwa anapopewa Rufaa kutoka kwenye ngazi ya msingi kwenda ngazi za juu," ameeleza.

Amewataka wananchi kuwa na programu maalumu za kujipangia maisha ambayo yanarefusha, kuongeza ubora wa maisha na kupunguza matatizo huku akiwataka kwenye ngazi ya familia kusisitizana,shuleni kupima na kufundisha kwenye mitaala kuhusiana na Shinikizo la juu la damu.

Amesema pia kazini, wafanyakazi waweke siku za kuhakikisha wanatangaza michezo, kukumbushana lishe ambayo inastahili ikiwa ni pamoja na kuweka misingi ya kujiliwaza na kupumzika kidogo ili kupunguza msongo wa mawazo ambao unachangia kuongeza Shinikizo la juu la damu.

WAZIRI WA AFYA 


Awali Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema wagonjwa wenye Shinikizo la juu la damu wameonekana kuongezeka takribani mara mbili zaidi kwa kipindi cha miaka mitano (Health Statistical Bulletin 2022 kutoka wagonjwa 688,901 mwaka 2017 hadi kufikia 1,345,847 mwaka 2021 sawa na asilimia 95.4.

Waziri Ummy ameeleza kuwa takwimu kutoka kwenye mfumo wa ukusanyaji taarifa za afya (DHID2),nchini Tanzania zinaonesha jumla ya wagonjwa 2,535,281 walitibiwa magonjwa yasiyoambukizwa kwenye vituo vya afya mwaka 2017, wagonjwa hao wameongezeka hadi kufikia 3,440708 mwaka 2021.

Ameongeza kuwa  ongezeko hilo la wagonjwa wako 905,427 kwa kipindi hicho cha miaka mitano sawa na ongezeko la asilimia 94.

Waziri Ummy ameeleza kuwa tangu Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ilipoanzishwa Septemba 2015 hadi Aprili 2023 kati ya wagonjwa 619,102 waliowatibia asilimia 66 ya wagonjwa walikuwa na tatizo la Shinikizo la juu la damu ikiwa na maana kila wagonjwa 10 wanaoonwa katika taasisi hiyo 6 wana ugonjwa huo.

Amesema uchunguzi uliofanywa katika jamii kwenye mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara,Lindi Iringa na Dar es salaam takwimu zinaonesha watu watatu hadi wanne kati ya 10 wana ugonjwa huo.

Waziri huyo amesema ugonjwa huu ndio sababu kubwa (vihatarishi) ya kihausi (Stroke), shambulio la moyo (Heart attack), moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure), kutuna kwa Kuta za mishipa ya damu, moyo,uharibifu kwenye chujio za figo, ganzi miguuni na mikononi, upofu na kupunguza nguvu za kiume kwa wanaume.

"Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dk. Samia inaendelea na utekelezaji wa sera ya afya ya mwaka 2007 ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu kwa umahiri zaidi, amesema Waziri Ummy.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI