COSTECH: SERIKALI YAIDHINISHA MIRADI YENYE THAMANI YA MILIONI 120


Na Asha mwakyonde, Dodoma 

SERIKALI kupitia Tume Taifa ya  Sayansi na Teknolojia (COSTECH), 
imeidhinisha miradi miwili yenye thamani ya shilingi milioni 120 kila mradi ambapo utekelezaji wake unahusisha watafiti kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini ambapo itafanyika ndani ya miaka miwili ambayo  ipo katika hatua ya kusaini mikataba.

Hayo yamesemwa leo Agosti 25,  jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Amos Nungu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa Tume hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mkurugenzi huyo amesema mwaka wa fedha 2022/2023, Tume kwa kuzingatia vipaumbele ilivyojiwekea, ilijikita kutekeleza majukumu mahsusi ambayo ni kuratibu, kukuza na kuendeleza utafiti,kuratibu, kuendeleza na kuhawilisha teknolojia na ubunifu na kukusanya, kuhifadhi na kusambaza taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

Amesema serikali ilifadhili miradi ya utafiti kupitia COSTECH, baadhi ya miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na Tume inafanya ufuatiliaji wa miradi inayohusu kuboresha maabara za utafiti kwa ukarabati na ununuzi wa vifaa vya kisasa ikiwemo, Maabara ya Utafiti wa Baharini katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar mradi ambao tayari ulishakamilika.

"Mradi mwingine ni maabara ya chanjo ya mifugo katika Taasisi ya Taifa ya Chanzo, Maabara ya Afya ya Udongo ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, mtambo wa kutengeneza Mvinyo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, Makutopora na Maabara ya Kisasa ya Utafiti wa Mbogamboga na Matunda kwenye Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Kilimo," amesema.


Ameongeza kuwa Tume hiyo ina mashirikiano na Mabaraza ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STU) ya nchi 17 za kusini mwa Jangwa la Sahara (SGCI), baadhi ya raslimali fedha zilizoshindaniwa na kuletwa hapa nchini kupitia mabaraza hayo ni uanzishwaji wa Vigoda viwili vya utafiti vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 2, mradi huu utatekelezwa kwa miaka mitano ambapo kwa sasa ni mwaka wa pili. 

Kwa mujibu wa Nungu zaidi ya Dola za Marekani milioni 1 zimepatikana kwa ajili ya kufadhili tafiti mbalimbali zenye msisitizo wa mashirikiano kati ya Vyuo Vikuu na wadau wengine.

"COSTECH ni mwanachama wa Baraza la Utafiti Duniani, mwaka jana wanachama walikubaliana kuja na mradi wa majaribio wa utafiti wa pamoja ambapo Kamisheni kutoka nchi 11 zinashiriki andiko hilo kutoka mabara manne ikiwemo Afrika, hii inatoa fursa kwa watafiti wetu kujenga mahusiano, kujifunza na pia fursa ya kutumia vifaa vya kisasa kutoka kwa wenzetu,"ameeleza.

Amefafanua kuwa mradi wa majaribio wa utafiti wa pamoja unakusudiwa kuwa mradi wa miaka 2-4 ambapo imetengwa shilingi milioni 120 kwa kila mradi na Tume inakusudia kufadhili miradi minne, kwa maana ya kufanikisha tafiti nne kushiriki. 

Nungu ameeleza kuwa Tume hiyo inatoa vibali vya utafiti kwa Watafiti kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi kupitia Kamati ya Kitaifa ya Kupokea na Kujadili Maombi ya Vibali vya Utafiti (NRCC), katika kipindi cha miaka mitano, zaidi ya vibali 3,000 vimetolewa ambapo tafiti zilizopata vibali zimejikita katika Sekta mbalimbali 

"Katika upande wa kuratibu, kuendeleza na kuhawilisha teknolojia na ubunifu, Tume iliendelea kuratibu shughuli na programu mbalimbali za ubunifu nchini ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa teknolojia, uanzishaji vituo mbalimbali vya ubunifu na kuwasaidia wabunifu," amesema.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI