WATAALAM 1,600 WA TEHAMA WASAJILIWA

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

TUME ya TEHAMA,imesema, ipo katika hatua za awali za ujenzi wa vituo vikubwa nane katika Mikoa mikubwa ambapo vituo hivyo vitakwenda kuongeza ujuzi kwenye maeneo mapya ya Wataalam hasa watakaobobea katika akili Bandia.

Pia hadi sasa Tume hiyo imeshasajili wataalam wa TEHAMA 1,600 wanaohudumia nchi nzima.

Hayo yamesemwa leo Agosti 25 ,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo,Dk.Nkundwe Mwasaga 
 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya TEHAMA na Mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, amesema baadhi ya mafanikio ya Tume ni kuanzishwa kwa mradi wa kujengwa kituo kikubwa cha Taifa cha Ubunifu Dar es s Salaam kwa ajili ya kutoa huduma kwa wataalam, watafiti, na wabunifu wa TEHAMA.

Amesema mafanikio mengine ni kuanzisha kituo kimoja cha ubunifu TEHAMA (Softcentre) Zanzibar, vinne vya Kanda katika majiji ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Tanga, Lindi na Mbeya kwa ajili ya kuendeleza kampuni changa za TEHAMA na kuendeleza kituo cha Dar es Salaam ili kukuza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa za TEHAMA na kukuza uchumi wa nchi.

"Tume pia imeanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya TEHAMA (ICT refurbishment and assembly centre),na kuwezesha mafunzo maalum ya TEHAMA kwa wataalam kukuza na kuendeleza ujuzi wa TEHAMA nchini," ameeleza.

Pamoja na hayo, Mwasaga  amebainisha kuwa Tume hiyo kwakushirikiana na Benki ya CRDB imefanya Uwekezaji kwaajili ya kampuni ndogo  za TEHAMA ambapo watakuwa wakitoa Shilingi Bilioni5 Kila Mwaka kwa lengo la kuhakikisha Vijana wanapata ajira.


Naye Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO Gerson Msigwa amesema Serikali imeamua kuwekeza kwa nguvu kwenye Tanzania ya Kidijitali chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambapo msimamizi mkuu unafanywa na Tume ya TEHAMA.

"Hili ni jambo kubwa kwani fedha nyingi imewekezwa kwa ajili ya kuboresha TEHAMA nchini kwani shughuli mbalimbali kwa sasa duniani zinafanyika kwa njia ya kidijitali ikiwemo huduma za malipo mabalimbali, huduma za afya za matibabu, uzalishaji, kilimo, uchimbaji wa madini," amesema.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU