DAR YAONGOZA MATUKIO YA KUNG'ATWA NA WANYAMA, SERIKALI YATOA DOZI 180,000

Na Asha Mwakyonde, Mpwapwa

MKOA wa Dar es salaam unaongoza kwa  kuwa na matukio ya watu kung'atwa na wanyama kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu ikifuatiwa na Dodoma, Morogoro na Arusha.

Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha mashirikiano na wadau mbalimbali kwa lengo la kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza leo Septemba 28,2023  katika Maadhimisho ya Siku ya Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika wilayani Mpwapwa jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu (OWM-SBU),Arbogust  Waryoba amesema kuwa Dar es salaam ina matukio 3,321,Dodoma 3,136, Morogoro 1,559 na Arusha 1,559 na kwamba takwimu hizo zinajumuisha wananchi waliopata huduma katika vituo vya afya.


Waryoba ameeleza kuwa ugonjwa huo hapa nchini uliripotiwa mara ya kwanza mwaka 1932 ambapo wagonjwa waliendelea kutolewa taarifa kutoka maeneo mbalimbali kwa kiwango tofauti.

Ameongeza kuwa serikali imechukua jukumu la uchanjaji wanyama mbwa na paka ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu isemayo 'Kichaa cha Mbwa Janga la Wote, Afya Moja kwa Wote'.

" Katika kipindi hiki cha maadhimisho jumla ya dozi 180,000 za chanjo ya kichaa cha mbwa zimesambazwa katika Halmashauri 26 nchini kuanzia Septemba 24 hadi kufikia leo Siku ya maadhimisho haya," amesema.

Kaimu Katibu huyo amefafanua kuwa mbwa 20,436 na paka 740 tayari wameshachanjwa katika Halmashauri hizo 26.

Aidha, amewashukuru wadau wanaoshirikiana na serikali katika kuunga mkono juhudi zake zikiwamo taasisi na mashirika yakiwamo Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Afya ya  Wanyama Duniani (WOAH), Ifakara Health Institute (IHI), na Global Animals Health.


Kawa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi Msaidizi wa afya ya mifugo ngazi ya jamii Dk.Stanford Ndibalema amesema ugonjwa wa kichaa cha mbwa unaishi  kwa baadhi ya wanyama wa porini  kama popo na baadae kwenda kwa mbwa.

"Kama tukiweza kuwakinga mbwa na paka kwa kuwachoma kuwachanja hii itasaidia  binadamu kutokupata ugonjwa wa kichaa cha mbwa," ameeleza Dk. Ndibalema.

Naye Mwakilishi wa Wizara ya Afya Robert Kishimba ameeleza kuwa wanashirikiana na sekta ya mifugo kuhakikisha wananchi wanakuwa salama kwa kuwapatia elimu.

"Tunapoacha kutekeleza yale tunayoshauriwa ina sababisha ugonjwa kuingia kwa wanyama hawa na baadae kwenda kwa binadamu," amesema Kishimba.

Ameongeza gharama ya kutibu, kuzuia ugonjwa huo ni nafuu kuliko kutibu mtu aliyeng'atwa na mbwa ambapo gharama yake ni kubwa.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA