WANANCHI KIJIJI CHA NGAHOKORA KUNUFAIKA NA NISHATI YA UMEME


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama ( katikati) akiwa ameketi katika moja ya madarasa ya mfano ya  Elimu ya Awali katika Shule ya Msingi Ngahokora iliyopo Kata ya Kizuka, Kijiji cha Ngahokora , Wilaya ya Songea Vijijini Mkoani Ruvuma  kuashiria uzinduzi wa madarasa hayo tayari kwa kutumika.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi kitanda cha kujifungulia kwa kina mama katika Zahanati ya Ngahokora wakati wa ziara yake Mkoani Ruvuma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na baadhi ya wakazi  wa  Kata ya Kizuka, Kijiji cha Ngahokora  ikiwa ni muendelezo wa ziara yake Wilaya ya Songea Vijijini Mkoani Ruvuma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali baada ya kuzindua  madarasa ya mfano ya  Elimu ya Awali katika Shule ya Msingi Ngahokora iliyopo Kata ya Kizuka, Kijiji cha Ngahokora , Wilaya ya Songea Vijijini Mkoani Ruuvuma  kuashiria uzinduzi wa madarasa hayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi vifaa vya michezo kwa  baadhi ya timu zilizopo katika  Kata ya Kizuka, Kijiji cha Ngahokora  ikiwa ni sehemu ya kuchangia sekta ya michezo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na Mwandishi wetu- RUVUMA

WWAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha linafikisha huduma ya umeme katika Kijiji cha Ngahokora kufikia  mwezi Desemba mwaka huu.

Mhe. Jenista ametoa agizo hilo mara baada ya kuzindua  madarasa ya mfano ya  Elimu ya Awali katika Shule ya Msingi Ngahokora iliyopo Kata ya Kizuka, Kijiji cha Ngahokora ,Wilaya ya Songea Vijijini ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma.

Ameeleza kuwa kufikishwa huduma hiyo muhimu itakuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo katika kujikwamua kiuchumi kwa sababu utasaidia katika shughuli za uzalishaji na matumizi ya nyumbani pamoja kusaidia katika huduma za afya pindi wananchi wanapoenda kupatiwa matibabu katika Zahanati na Vituo vya afya.

“Ilani ya Chama Cha Mapundizi (CCM) tunaitekeleza kwa miaka mitano na ndani ya mwaka wa pili  na sasa tunamalizia wa tatu mwaka 2021 umeme umefika Magagula kisha ukaelekea Kizuka na 2023 umeme utaelekea Mbilo na kisha hapa Ngahokora kwa sababu kama Serikali tunatambua umuhimu wa nishati hii muhimu katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia na Taifa,” Ameeleza Mhe. Jenista.

Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt  Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya  kwa  kujenga hospitali ya  Wilaya  iliyopo eneo la Mpitimbi ambapo  zaidi ya Bilioni mbili zimewekezwa katika ujenzi wa hospitali hiyo na kutoa wito kwa wananchi kuitumia kupata huduma.

“Wananchi wa Ngahokora nyie ni sehemu ya  wanufaika wa  ile hospitali ya Wilaya ya Mpitimbi zaidi ya Bilioni mbili zimewekezwa pale  kwani itawasaidia msitembee umbali mrefu kutafuta matibabu kutoka hapa Ngahokora ni rahisi kufika hospitali ya Mpitimbi kuliko kwenda Peramiho na niliwaahidi kutoa fedha ili kuunganisha barabara itakayoasaidia kufika kwa urahisi hapo Mpitimbi,” Amefafanua Waziri huyo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bw. Menas Komba amebainisha  kwamba kijiji hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto  mbalimbali zikiwemo barabara, maji, uhaba wa vitanda vya kujifungulia kwa  kina mama , umeme  pamoja na mawasiliano lakini Serikali imeendelea kuzitatua kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu na kufanya shughuli za  uzalishaji.

Aidha Diwani wa Kata ya Kizuka Mhe. Jacob Nditi amebainisha kwamba utekelezwaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayofanywa na Serikali katika Kijiji hicho inaonyesha nia njema ya Serikali  ya Awamu ya Sita ya  kuwaletea wananchi wake maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji  wa  Kijiji  cha Ngahokora Bi. Tumaini Kaaya ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundo mbinu ya elimu akisema kuwa kukamilika kwa madarasa hayo kutatoa mwamko kwa wazazi  kupeleka watoto shule na wanafunzi kujifunza katika mazingira rafiki.

“Tunaishukuru serikali kwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika kijiji chetu, Mhe. Mbunge kwa kutupatia madarasa mawili ya mfano ya  elimu ya awali, madarasa mawili ya shule ya msingi Ngahokora, tunaishukuru TARURA kwa kuanza kuondoa visiki ili kuchonga barabara na TANESCO kutuongeza nguzo 53 ili kutuletea  huduma ya umeme,” Ameshukuru Afisa huyo.

Nao baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Msingi Ngahokora wakisoma risala yao  wameeleza kwamba kujengwa kwa madarasa hayo kwao ni chachu kubwa ya kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao huku wakimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya elimu.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI