Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Umoja wa watoa Huduma za mawasiliano wamesaini hati ya maridhiano na hati ya mkataba wa nyongeza kwenye miundombinu ya mkongo wa mawasiliano.
Utiaji Saini wa hati hiyo na mkabata huo ni maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kutatuliwa kwa mgogoro uliokuwepo kati ya umoja huo na serikali jambo lililosababisha kukwama kwa shughuli za uwekezaji ili sekta kuwa wezeshi na kuchangia uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa leo Septemba 25,2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye katika hafla ya utiaji saini hati ya maridhiano na hati ya mkataba wa nyongeza kwenye miundombinu ya mkongo wa mawasiliano amesema lengo ni kuweka mazingira wezeshi kwa makampuni ya kutoa huduma ya mawasiliano ili kuongeza wigo katika sekta hiyo.
Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Umoja wa watoa huduma na wawekezaji kujenga miundombinu ya Mawasiliano kote Nchini na wakahakikishia tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha.
Aidha ameyataka makampuni ya kutoa huduma za mawasiliano kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ili kufikia wananchi wengi zaidi pamoja huku akiwasisitiza mikataba hiyo izingatie utekelezaji utakaoonesha matokeo.
" Endapo itatokea uzembe hatua zichukuliwe mapema kabla ya kufikia migogoro, tunatambua umuhimu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), amesema Waziri Nape.
Waziri Nape amesema miongoni mwa juhudi za serikali katika mawasiliano ni kumepunguza gharama za kuweka miundombinu ya mkongo kutoka Shilingi milioni 2.5 hadi kufikia 250,000.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa ambao unatarajia kuzifikia wilaya 99 kati 139 ifikapo machi 2024 huku lengo likiwa ni kufikia wilaya zote ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024.
0 Comments