Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WAFANYABIASHARA wametakiwa
kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan mwenye matarajio makubwa na maendeleo ya nchi kwa kulipa kodi na kwamba maendeleo hayawezi kufikiwa bila watu, wafanyabiashara kulipa kodi.
Pia wametakiwa kuwa wabobezi kwenye ajenda ya ulipaji kodi kwa kutumia Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD), lengo likiwa ni kutunza kumbukumbu za mauzo huku akiwaomba wafanyabiashara hao kuwahamasisha wengine ambao hawazitumii mashine hizo.
Hayo amesemwa jijini Dodoma leo Disemba 5,2023 na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri katika Siku ya shukurani kwa mlipa kodi
iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Dodoma alisema kutokulipa kodi ni kujizulumu.
Amesema kuwa siku ni ya kipekee na ya shukurani kwa walipakodi wa Dodoma kwa kuwatambua mchango wa wafanyabiashara walioutoa kwa serikali na Mkoa katika mwaka wa fedha 2022/2023,
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa hivi karibuni walikuwa na Baraza la Biashara mkoani hapo moja hoja zilozungumzwa ni kuanguka kwa biashara ambazo zinafanywa kienyeji kwa kukwepa kulipa kodi.
Ameongeza kuwa moja ya hasara za kutokulipa kodi ni kushindwa kupata mikopo mikubwa kutoka katika taasisi za kifedha.
"Kama mtu unakwepa kulipa kodi huwezi kuzipata fursa za kukopeshwa kwa kuwa unakwepa kodi, kiuhalisia unatakiwa ukopeshwe milioni 100 lakini huwezi kupata ndio maana unakuta mtu anabaishara hiyo hiyo miaka 10 hawezi kubadilika," ameongeza.
"Kutokulipa kodi ni kujizulumu wewe mwenyewe hivyo tuhamasishane sote na kujenga tabia zaidi ya kulipa kodi kuliko kupingana na sheria," amesema Mkuu huyo wa Dodoma Shekimweri.
Naye Meneja wa Mamlaka hiyo Mkoa wa Dodoma Castro John
amewataka wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati ambapo mwezi Disemba ni wa kulipa kodi awamu ya nne na kwamba ifikapo 31,mwezi huo wafanyabiashara hao wawe wameshalipa kodi.
amesema kuwa wafanyabiashara ni sehemu ya mchakato wa maendeleo ya Taifa na kwamba wasipokuwa timu moja katika ulipaji kodi nchi haiwezi kusogea mbele kiuchumi.
John amesema Mkoa wa Dodoma unajivunia kuwahudumia walipakodi na wafanyabiashara huku akisema ofisi zao zipo wazi muda wote na kwamba endapo wanachangamoto wafike ili kuzungumza.
" Kwa wale wenye changamoto ya matumizi ya mashine za EFDs waje tuzungunze, matumizi ya mashine hizi ni muhimu kwa kutunza kumbukumbu na kuleta makadirio ya kodi sahihi," ameeleza.
Ameongeza kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wafanyabiashara kulalamika kodi kubwa na wanapoambiwa wapeleke kumbukumbu zao wanakuwa hawana na kwamba matumizi ya sahihi ya mashine hizi yanasababisha makadirio kuwa sahihi.
"Leo ni siku ya kipekee ni ya shukurani kwa walipakodi wa Dodoma kwa kuwatambua mchango wa wafanyabiashara hawa walioutoa kwa serikali na Mkoa katika mwaka wa fedha 2022/2023 lakini pia niwashukuru waandishi wa habari tumekuwa tukifanya kazi pamoja," ameeleza.
Ameongeza kuwa siku hiyo ni muhimu kwa TRA ambayo inawatambua walipakodi ambapo asubuhi walifanya matembezi ya shukurani kwa ajili ya wafanyabiashara hao na kufuatiwa na hafla fupi jioni ya kuwatunuku waliofanya vizuri katika suala la ulipaji kodi.
Meneja huyo amesema kuwa wafanyabiashara wote mkoani hapo wamefanya vizuri katika ulipaji kodi na kwamba watakaotunukiwa ni wale waliofanya vizuri zaidi ili iwe chachu kwa wengine.
Kwa upande mwakilishi wa wafanyabiashara Mkoa wa Dodoma Joseph Chowa amempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ya ulipaji wa kodi.
" Tunaomba matumizi sahihi na mazuri ya vitendea kazi vya ukusanyaji kodi kama mashine za EFDs kusaidia kuleta taarifa zetu ili kuepuka malalamiko ya kodi zinazotukabili," amesema.
Aidha mfanyabiashara huyo aliwashauri wafanyabiashara wengine kutimiza majukumu yao ya kulipa kodi sahihi inayostahili na kuacha kukwepa ulipaji wa kodi hiyo huku akifafanua kuwa kodi ni jukumu la mfanyabiashara yoyote katika kujenga Taifa kwa pamoja.
Katika siku hiyo muhimu Mamlaka hiyo imetembelea Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe na kutoa msaada mbalimbali zikiwamo sabauni, taulo za kike.
Akizungumzia katika Hospitali hiyo Kaimu Mkurugenzi Mirembe Innocent Mungoki ameishukuru serikali kwa mwaka wa fedha 2023 suala la Afya limepewa kipaumbele na TRA na kwamba wao wanaendelea kuonyesha kwa vitendo.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka hiyo John amesema kuwa kuzingatia maadhimisho ya siku ya mlipa kodi wameona siyo vibaya kuhakikisha wanawafikia ndugu zao ili na wao wajione ni sehemu ya jamii.
0 Comments