Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akijibu swali Bungeni leo tarehe 08 Februari 2024 Jijini Dodoma.
Na Mwandishi wetu- DODOMA
Serikali imesema imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa ikiwemo Kuandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Nino kwa kipindi cha mwezi Septemba 2023 mpaka mwezi Juni 2024.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga Bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 08 Februari 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mwera Mhe. Zahor Mohamed Jaji aliyetaka kufahamu kuhusu athari za mvua zilizonyesha Novemba, 2023 na mpango wa Serikali kuzuia athari hizo kujirudia.
Mhe. Ummy ameongeza kuwa Ofsi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa inaendelea kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa katika Mikoa 18 nchini, kufuatilia mwenendo wa majanga, kutoa tahadhari kwa umma kupitia Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura.
“Ili kukabiliana na athari hizi, Serikali imechukua hatua mbalimbali kama vile kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia utekelezaji wa mikakati na mikataba ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo Mkakati wa Kimataifa wa Sendai wa Upunguzaji wa Athari za Maafa (2015-2030) na Mkataba wa Makubaliano wa kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Oparesheni za Dharura cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (2022),”Alisema Mhe. Ummy.
Akiyataja baadhi ya madhara katika yaliyotokana na mvua zilizonyesha katika kipindi cha kuanzia Mwezi Oktoba, 2023 hadi sasa, amebainisha kwamba ni pamoja na mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya milipuko kwa binadamu ikiwemo kipindupindu, matukio ya radi pamoja na upepo mkali ambayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali.
Aidha akijibu swali kuhusu namna Vijana wenye Ulemavu walivyonufaika na mafunzo na mikopo inayotolewa na Serikali Naibu Waziri Ummy ameeleza kwamba kwa mwaka wa fedha 2022/2023, zaidi ya vijana 2000 wamenufaika na mafunzo yanayotolewa hapa nchini kupitia ufundi stadi na ujasiriamali katika Vyuo vya ufundi stadi na marekebisho, vyuo vya VETA na programu ya ukuzaji ujuzi iliyopo Nchini.
“Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi cha Mwaka 2022, kiasi cha mikopo ya Shilingi bilioni 81.3 zilizotolewa kwa watu 640,723 wenye ulemavu wakiwemo vijana wenye ulemavu ili kuwezesha vijana wenye ulemavu kuanzisha au kuendeleza biashara zao hivyo kupunguza utegemezi,” Alifafanua Mhe. Ummy.
0 Comments