SERIKALI YASAINI MIKATABA UPEMBUZI YAKINIFU UNUNUZI MELI NA UJENZI WA VIWANDA


Na Asha Mwakyonde, Dodoma

SERIKALI imesema kuwa katika zoezi  la upembuzi yakinifu la programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), italisimamia kwa ukaribu ili kuhakikisha linafanyika kwa ufanisi unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zote zitakazojitokeza.

Hayo yalisemwa leo Februari 27,2024  jijini Dodoma na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi  wakati wa halfa ya utiaji saini wa mikataba wa Upembuzi Yakinifu wa ununuzi wa Meli  nane za Uvuvi na ujenzi wa viwanda viwili vya kuchakata Samaki Kilwa na Fungurefu kupitia programu ya AFDP amesema mkataba huo utatekelezwa kwa muda za siku zisizozidi 45 kwa gharama ya Shilingi milioni 348.

Katibu Mkuu huyo amefafanua kuwa kukamilika kwa upembumbuzi yakinifu kwa wakati kutawezesha Serikali kuanza taratibu za ujenzi wa meli za uvuvi katika bahari kuu pamoja na viwanda vya kuchakata samaki.


" Nawahisi wakati wa utekelezaji wa zoezi hili la Upembuzi Yakinifu, mara watakapopata changamoto yoyote, tafadhali msisite kuwasiliana na ofisi yangu kwa utatuzi wa haraka ili tuweze kukamilisha zoezi ndani ya muda tuliokubaliana.Ni matarajio yetu kuwa hamtachelewesha utaratibu huo kuanza kwa wakati," amesema.

Amesema ni vyema wakafahamu hiyo  ni moja ya Programu za kitaifa za kimkakati zilizo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 2025/26 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Dk. Yonazi ameeleza kuwa ni programu ambayo Viongozi wakuu, Rais Dk. Samia na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi, wanaifuatilia kwa karibu lengo ni kuimarisha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa, pamoja na kuendeleza uchumi wa buluu.


"Mkifanya kazi hii kwa weledi na kukamilisha kwa wakati uliopangwa mtakuwa mmeshiriki katika kutafisiri maono ya Viongozi wetu hawa wakuu," ameeleza Katibu Mkuu huyo.

Kwa upande Mratibu wa programu hiyo Salimu Mwinjaka amesema kuwa programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), ni ya miaka sita ambayo ilianza mwaka 2021/2022 hadi 2027/ 2028 na itagharimu jumla ya dola za Kimarekani milioni 77.4.

"Kati ya fedha hizi mkopo kutoka IFAD ni dola za Marekani milioni 58.8, serikali dola za Marekani milioni 7.8, sekta binafisi dola za Marekani milioni 8.5 na wananchi dola za Marekani milioni 2.4, " amesema.

Ameongeza kuwa lengo la programu hiyo ni kuwa na uzalishaji endelevue wa kibiashara na wenye kuzingatia mazingira hususan uzalishaji wa mbegu za mazao ya Kilimo kama mahindi, alizeti maharage na mimea ya mikunde, uvuvi na ufugaji wa viumbe maji ambao unazingatia uwezeshaji wa akina mama na ushiriki wa vijana.


Mratibu huyo ameeleza kuwa programu hiyo inatarajia kuwanufaisha watu trakibani 1,300,000 ikiwamo kaya Wakulima wadogo 200,000 ambao watakuwa wanapata mbegu bora za mahindi,alizeti na maharage.

Aidha amesema kuwa Upembuzi Yakinifu wa awali  tayari umefanyika na kubainisha Meli hizo zitaleta tija kwa uchumi na kwamba katika Upembuzi Yakinifu huo umependekeza Meli ziwe na urefu wa mita 26 na kuingia mkataba na 
Kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG).

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI