GCLA YAWEZESHWA BILIONI 4.57 KUNUNUA VIFAA VYA MAABARA,YATOA USHAHIDI WA KITAALAM MAHAKAMANI MASHAURI 882


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu ameeleza katika kuchangia utoaji wa haki katika vyombo vya maamuzi kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imetoa ushahidi wa kitaalam mahakamani kwa mashauri 882 sawa na asilimia 71.4 ya lengo la kutoa ushahidi wa mashauri 1,236. 

Amesema katika kuhakikisha kuwa Mamlaka inakuwa na Vifaa vya kutosha kulingana na mahitaji na vyenye teknolojia ya kisasa, Serikali imeiwezesha kununua mitambo mikubwa mitatu aina ya Gas Chromatography Mass Spectrometer (GC-MS/MS), MinLab 153 (OSA4) na Gas Chromatography (GC) pamoja na vifaa vingine vya maabara vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.57 na kwamba uwekezaji huo umeiwezesha kuwa na ufanisi na kuendelea kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi.

Akiwasilisha hotuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni leo Aprili 13,2024Jijini hapa Waziri Ummy amesema kulikuwa na ongezeko la asilimia 117 ikilinganishwa na mashauri 407 yaliyotolewa ushahidi mahakamani kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/2023. 

Waziri huyo ameeleza kuwa mafanikio haya yamechangiwa na Mfumo wa Kielekitroniki wa Kuratibu Taarifa za Wataalam Watoa ushahidi Mahakamani - Expert Witness Management Information System.

Ameeleza kuwa Mamlaka hiyo katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 iliendelea kutoa huduma ya uchunguzi wa Kimaabara wa sampuli mbalimbali na vielelezo ambapo jumla ya sampuli 145,273 zilipokelewa. 

"Kati ya sampuli hizi, sampuli 141,683 zilifanyiwa uchunguzi sawa na asilimia 97.6 ya sampuli zilizopokelewa," amesema Waziri Ummy.

Amefafanua kuwa sampuli zilizofanyiwa uchunguzi ni sawa na ongezeko la asilimia 43 ikilinganishwa na sampuli 99,159zilizochunguzwa kwa kipindi kama hicho cha Mwaka wa Fedha 2022/23.

Waziri Ummy amesema matokeo ya uchunguzi huo yalisaidia Serikali na Mamlaka nyingine za usimamizi na udhibiti kufanya maamuzi stahiki katika kulinda afya za wananchi na mazingira pamoja na utoaji wa haki katika vyombo vya maamuzi. 

Amesema katika kuhakikisha ubora wa matokeo ya uchunguzi yanayokubalika kitaifa na kimataifa, Mamlaka imepata Ithibati ya Mifumo ya Ubora ya Maabara (ISO 17025:2017) katika Maabara ya Sayansi Jinai Toksikolojia.

Akizungumzia usajili Waziri Ummy amebainisha kuwa Mamlaka ilisajili wadau 974 wanaojishughulisha na biashara ya kemikali sawa na asilimia 82.8 ya lengo la kusajili wadau 1176. Wadau waliosajiliwa waliongezeka kwa asilimia 33.2 ikilinganishwa na Wadau 731 waliosajiliwa kwa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2022/2023. 

Waziri huyo amesema lengo la kusajili wadau hawa ni kuendelea na juhudii za kulinda afya, mazingira na usalama wa nchi dhidi ya kemikali hatarishi na bashirifu zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya au silaha za kemikali.

"Mamlaka pia ilitoa mafunzo kwa jumla ya madereva 2,961 juu ya usafirishaji salama wa Kemikali nchini na mafunzo haya yamesaidia kuwapa uelewa wa namna bora ya kujilinda, kulinda watu wengine pamoja na kulinda mazingira wakati wa usafirishaji wa kemikali hizo," amesema.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) ni taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya, iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Sura 177 yenye majukumu makuu ya kufanya uchunguzi wa Kimaabara wa sampuli mbalimbali na vielelezo, utoaji ushahidi wa kitaalam mahakamani na usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani nchini.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU