TMDA IMEENDELEA KULINDA MIPAKA KUZUIA UINGINZWAJI BIDHAA DINI,YATEKETEZA BIDHAA ZENYE THAMANI YA BILIONI 10.5


Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imesema kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imeendelea kulinda mipaka ya nchi kwa kuzuia 
uingizwaji wa bidhaa duni, bandia na ambazo hazijasajiliwa kwa kufanya doria na ukaguzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola.

Pia imesema katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi 2024 TMDA iliteketeza jumla ya tani 1,846.3 za bidhaa mbalimbali zenye thamani ya takriban Shilingi bilioni 10.5 na hivyo kuzuia bidhaa zenye madhara kuweza kumfikia mwananchi.

Akiwasilisha hotuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni leo Aprili 13,2024Jijini hapa Waziri Ummy Mwalimu amesema katika kuhakikisha Serikali inamlinda mwananchi dhidi ya matumizi ya 
bidhaa za afya ambazo hazikidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi na hivyo kutokuwa salama kwa matumizi ya binadamu, TMDA hufanya kaguzi za bidhaa mbalimbali za afya.

Waziri huyo amefafanua palinapobainika bidhaa hizo hazijakidhi vigezo huteketezwa ili kuepusha bidhaa duni, bandia na hafifu zisitumiwe na wananchi.

Ameeleza kuwa katika kuhakikisha usalama, ubora na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na vipukusi na hatimaye kulinda afya ya jamii, kati ya maombi 1,615 ya dawa za binadamu yaliyokuwepo katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024. 

Kwa mujibu wa Waziri Ummy Mamlaka ilitathmini maombi 1,175 ikiwa ni ongezeko la maombi 315 sawa na asilimia 36.6 ikilinganishwa na maombi 860 yaliyofanyiwa tathmini katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23. Kati ya maombi yaliyofanyiwa tathmini, maombi 660 yaliidhinishwa na kusajiliwa.

 "Jumla ya maombi 199 ya usajili wa dawa za mifugo yalipokelewa ambapo maombi 129 yalifanyiwa tathmini na maombi 95 yaliidhinishwa baada ya 
kukidhi vigezo. 


Amesema katika kuhakikisha usalama, ubora na ufanisi wa vifaa tiba navitendanishi, kati ya maombi 221 ya usajili wa vifaa tiba na vitendanishi maombi 201 yalifanyiwa tathmini na jumla ya maombi 145 yaliidhinishwa.

Waziri huyo ameongeza kuongezeka kwa idadi ya bidhaa zinazokidhi viwango na kusajiliwa ni kiashiria kuwa wafanyabiashara wameendelea kuzingatia matakwa ya kisheria.

Akizungumzia madhara ya kutambua yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa za tumbaku, ameeleza kuwa mamlaka hiyo imepewa jukumu la kudhibiti uzalishaji, usambazaji, matangazo na mauzo ya bidhaa za tumbaku.

" Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 ukaguzi wa maeneo 117 yanayojihusisha na uendeshaji wa biashara ya bidhaa za tumbaku ulifanyika ambapo yote yalikidhi 
vigezo pia TMDA ilifanya ukaguzi wa shehena tatu za vifungashio vya bidhaa za tumbaku zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 2.2 katika vituo vya forodha,"ameeleza.

Ameongeza kuwa bidhaa za tumbaku zenye uzito wa tani 0.11 na thamani ya takriban Shilingi157,358,940.22 ziliteketezwa baada ya kubainika 
kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu. 

Waziri Ummy amebainisha kuwa katika kipindi hiki kulikuwa na maombi 379 ya usajili wa maeneo ya biashara zinazohusiana na dawa ambapo maombi 369 sawa na asilimia 99 yalifanyiwa tathmini ambapo 347 sawa na asilimia 94 yalikidhi vigezo vya usajili na hivyo kupewa vibali vya biashara.

Amesema maombi 457 ya 
usajili wa maeneo ya biashara zinazohusiana na vifaatiba na vitendanishi yalipokelewa ambapo 450 yalitathminiwa na maeneo 448 sawa na asilimia 99 yalikidhi vigezo na hivyo kusajiliwa. Aidha, TMDA ilifanya ukaguzi wa maeneo 7,693 ya biashara ya bidhaa zinazohusiana na dawa nchini ambapo maeneo 6,727 sawa na asilimia 87 yalikidhi vigezo. 

"Ukaguzi wa viwanda 139 ndani na nje ya nchi ulifanyika katika kipindi hiki ili kuhakikisha kuwa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinatengenezwa kwa kufuata taratibu za utengenezaji bora (GMP) na hivyo kuwalinda watumiaji," amesema.

TMDA ni taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya, imeanzishwa chini ya Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219 yenye jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kuhakiki ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa zitokanazo na tumbaku. 

Pia ilianzishwa ikiwa na lengo la 
kuongeza tija na ufanisi katika udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI