WAZIRI AWESO: TAARIFA YA UTENDAJI EWURA IMEBAINI MAFANIKIO ONGEZEKO LA UZALISHAJI MAJI LITA BILIONI 7


Na Asha Mwakyonde,Dodoma

SERIKALI Kupitia wizara ya maji imesema kuwa mwaka 2022/2023, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),ilitoa taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira na ambapo ilibaini kuwepo kwa mafanikio katika ongezeko la uzalishaji wa maji kwa lita bilioni 7 sawa na asilimia 1.78.

Pia EWURA ilibaini kuongezeka kwa uwezo wa miundombinu ya kuzalisha maji kwa lita bilioni 126 sawa na asilimia 16.94 na kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaopata huduma ya maji kwa asilimia 11. 

Akiwasilisha hotuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni leo Mei 9, 2024 Jijini Dodoma, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema kuwa taarifa hiyo inaainisha utendaji wa mamlaka za maji nchini na kuweza kusaidia Wizara pamoja na wadau wa sekta ya maji katika kuandaa na kutekeleza mipango mbalimbali ya kuimarisha na kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira.

Waziri huyo ameeleza kuwa EWURA taarifa imebainisha changamoto zinazokabili mamlaka za maji zikiwemo, kuongezeka kwa upotevu wa maji ambao umefikia asilimia 37, upungufu wa miundombinu ya huduma ya usafi wa mazingira; na uwiano usioridhisha wa ongezeko la mahitaji ya maji ikilinganishwa na uzalishaji wa maji.

Amesema hadi mwezi Aprili 2024, EWURA ilitoa leseni nne za kutoa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Miji ya Rombo, KyelaKasumulu, Njombe na Busega. 

"EWURA ilitathmini na kuidhinisha bei mpya za huduma ya maji kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira saba ambazo ni Dodoma, Makonde, Sumbawanga, Orkesumet, Mombo, Bariadi na Lindi," amesema Waziri Aweso.

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho, EWURA ilifanya mapitio ya mipangobiashara ya mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 11 na kuidhinisha mikataba sita ya huduma kwa mteja kwa mamlaka za Musoma, Liwale, Makambako, Lindi, Biharamulo na Geita.

Akizungumzia huduma za maji mijini ameeleza kuwa zinadhibitiwa na EWURA kupitia Kifungu namba 414 cha Sheria Namba .11 ya Mamlaka hiyo ya mwaka 2001. 

"Sheria hii inaitaka EWURA kudhibiti utoaji wa huduma kwenye Sekta za Maji na Nishati katika maeneo ya maji na usafi wa mazingira, umeme, mafuta ya petroli pamoja na gesi asilia," ameeleza Waziri huyo.

Ameongeza kuwa majukumu ya EWURA ni pamoja na kutoa leseni, kusimamia utekelezaji wa masharti ya leseni, kudhibiti ubora na ufanisi wa utoaji huduma, kutathmini na kupitisha bei za huduma na kutatua migogoro baina ya watoa hudumana wateja wao.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI