WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAWANUFAISHA WANANCHI ZAIDI YA 200 KUPITIA MSAADA WA KISHERIA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA


Utoaji wa Elimu ya Kisheria Watajwa Kuimarisha Upatikanaji wa Haki kwa Wananchi

Na Mwandishi wetu, DODOMA

ZAIDI ya wananchi 200 wamepata huduma za msaada wa kisheria na elimu kuhusu haki zao kupitia banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyohitimishwa leo Juni 23,2026 katika Viwanja vya Chinangali Park jijini hapa.

Huduma hizo zimewawezesha wananchi kupata ushauri wa kisheria, kuuliza maswali mbalimbali yanayowakabili na kufahamishwa haki zao za msingi, taratibu za kisheria pamoja na namna ya kupata msaada wa kisheria wanapouhitaji.

Hayo yameelezwa mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Moses Kasiluka, wakati alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Baada ya kupokea maelezo kutoka kwa wataalamu wa wizara hiyo, Prof. Shemdoe aliipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa juhudi kubwa inazoendelea kuzifanya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisheria kwa urahisi, hatua inayochangia kuongeza uelewa kuhusu haki zao na taratibu mbalimbali za kisheria.

Amesema huduma zinazotolewa na wizara hiyo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanaokumbana na changamoto mbalimbali za kisheria, huku akibainisha kuwa uwepo wa wataalamu katika maonesho hayo umefungua fursa kwa wananchi kupata ushauri na mwongozo wa haraka kuhusu masuala yanayowakabili.

Prof. Shemdoe ameishauri Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za umma pamoja na wadau mbalimbali walio karibu na wananchi ili kurahisisha utoaji wa huduma za kisheria na kupunguza changamoto zinazowafikisha wananchi katika ngazi za juu za Serikali.

Aidha, ameeleza kuwa changamoto nyingi zinazowasilishwa katika Wizara ya Katiba na Sheria mara nyingi huanzia katika taasisi au ofisi nyingine za Umma, hivyo kuna umuhimu wa kujenga mifumo madhubuti ya ushirikiano, uratibu na utatuzi wa changamoto hizo katika ngazi za awali kabla hazijafikia wizara husika.

Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kuokoa muda na gharama kwa wananchi, pamoja na kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za Serikali zinazohusika na utoaji wa huduma mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments

SERIKALI YAJIPANGA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO