Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MAFANIKIO ya kijana mbunifu mwenye ulemavu wa mikono anayebuni ramani za majengo na samani kwa kutumia miguu kupitia kompyuta mpakato Joseph Mtei, yamesababisha Serikali kuipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), huju ikisema taasisi hiyo imekuwa chachu ya kuibua vipaji na kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kupitia stadi za kazi.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, leo Juni 23,2026 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Prof. Shemdoe, amesema mafanikio ya kijana Mtei mwenye ulemavu aliyepata mafunzo kupitia VETA na kubobea katika usanifu wa majengo kwa kutumia mifumo ya kompyuta, ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa na taasisi hiyo katika kuwawezesha vijana kujitegemea kupitia ujuzi wa kazi.
Amesema Serikali imevutiwa na uwezo mkubwa alionao kijana huyo na namna alivyoweza kutumia mafunzo aliyoyapata kujijengea taaluma inayoweza kumuwezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.
VETA imekuwa na mchango mkubwa katika kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wenye ulemavu, hatua inayowapa fursa za ajira na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa.
“Nimepata nafasi ya kuzungumza na kijana huyu wakati wa kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kujionea kiwango kikubwa cha ubunifu na utaalamu alionao katika kazi za usanifu wa majengo. Nimejiridhisha kuwa ana uwezo mkubwa sana na ni mfano wa vipaji vilivyopo nchini ambavyo vinahitaji kuibuliwa na kuendelezwa,” amesema Prof. Shemdoe.
Ameongeza kuwa mafanikio ya Joseph yanaonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi stadi kwa vijana wenye mahitaji maalum ili kuwapa nafasi sawa za kushiriki katika maendeleo ya taifa.
Prof. Shemdoe p ameipongeza VETA kwa kuendelea kuwafikia vijana wenye ulemavu na kuwapatia stadi za maisha zinazowawezesha kujiajiri au kupata ajira katika sekta mbalimbali.
Aidha, amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhakikisha Joseph anatafutiwa ufadhili wa masomo ili aweze kuendelea kujiendeleza katika taaluma ya teknolojia na usanifu wa majengo.
Mbali na hilo, Prof. Shemdoe amesema alielezwa kuwa kwa sasa kijana huyo anafanya kazi VETA kwa mkataba, hivyo akaelekeza kuanza kwa mchakato wa kumpatia ajira ya kudumu serikalini kutokana na umahiri na uwezo mkubwa aliouonesha.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za taasisi mbalimbali zinazowezesha makundi maalum kupata elimu, mafunzo na fursa za ajira kwa lengo la kujenga jamii jumuishi na yenye usawa wa fursa kwa wote.




0 Comments