TMA YAHAMASISHA MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KATIKA MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA


 Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) , imeendelea kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa wananchi na wadau mbalimbali kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.

Akizungumza katika banda la Mamlaka hiyo Afisa Masoko wa Makutoka TMA Nasry Msulwa amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kuhusu huduma za hali ya hewa, ikiwemo utabiri wa kila siku, utabiri wa msimu, tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa pamoja na mchango wa taarifa hizo katika kusaidia sekta mbalimbali kufanya maamuzi sahihi.

Msulwa ameeleza kuwa maonesho hayo, mamlaka hiyo imejikita katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za hali ya hewa kwa wakati ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matukio mbalimbali yanayohusiana na hali ya hewa.

Amesema sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, usafiri wa anga na majini pamoja na usimamizi wa maafa ni miongoni mwa sekta zinazotegemea kwa kiwango kikubwa taarifa za hali ya hewa katika kupanga na kutekeleza shughuli zake.

Mbali na kutoa elimu ameongeza kuwa,TMA imeonesha teknolojia na mifumo inayotumika katika ukusanyaji, uchambuzi na utoaji wa taarifa za hali ya hewa, hatua inayowasaidia wananchi kuelewa mchakato mzima wa utoaji wa utabiri na tahadhari mbalimbali.

Wananchi waliotembelea banda hilo wamepongeza jitihada za TMA za kuendelea kutoa elimu kwa Umma, wakisema taarifa za hali ya hewa zimekuwa msaada mkubwa katika kupanga shughuli zao za kila siku na kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ushiriki wa TMA katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni sehemu ya jitihada za serikali za kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Umma.







Post a Comment

0 Comments

TMA YAHAMASISHA MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KATIKA MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA