Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),imesema inaendelea kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na usimamizi madhubuti wa viwanja vya ndege, hatua zinazochangia kukuza uchumi na kuimarisha huduma kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TAA, Irene Minja, wakati wa Maadhimisho na Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Minja amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu” inaakisi dhamira ya TAA ya kuhakikisha wananchi na wadau wanapata huduma bora zinazozingatia uwazi, uwajibikaji, usalama na ufanisi.
Ameeleza kuwa TAA ina jukumu la kujenga, kuendeleza, kusimamia na kuendesha viwanja vya ndege vya Serikali Tanzania Bara, na kwamba mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya sekta ya usafiri wa anga.
Kwa mujibu wa Minja, maboresho yanayofanyika katika viwanja vya ndege yanachochea ukuaji wa sekta nyingine muhimu za uchumi ikiwemo biashara, utalii na uwekezaji, huku yakiiwezesha Tanzania kuendelea kuunganishwa kwa urahisi na mataifa mbalimbali duniani.
“Tunatambua mchango mkubwa wa viwanja vya ndege katika maendeleo ya Taifa, ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma ili kuongeza ufanisi na kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha watalii, wafanyabiashara na wawekezaji,” amesema.
Aidha, amewahimiza wananchi kutembelea banda la TAA katika maonesho hayo ili kujifunza zaidi kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo, miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa umma.
Amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa taasisi za umma kusogeza huduma karibu na wananchi, kupokea maoni yao na kuimarisha uwajibikaji katika utoaji wa huduma bora na endelevu.



0 Comments