QWARAY: UJUZI WA VETA NI NGUZO YA AJIRA NA MAENDELEO

VETA yatajwa kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kwa mchango wake mkubwa katika kuwajengea vijana na makundi mbalimbali ya jamii ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Qwaray ametoa pongezi hizo leo Juni 22, 2026, alipotembelea banda la VETA katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo, Naibu Waziri ameeleza kuridhishwa na kazi inayofanywa na VETA katika kutoa mafunzo kwa watu wenye mahitaji maalum pamoja na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kupitia kampuni tanzu ya VETA ya Ujuzi.

“Niwapongeze kwa kuongeza ujuzi kwa vijana wetu kwani kupitia ujuzi huo wanaweza kujiajiri wenyewe.

Kwa sasa Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuwawezesha vijana kujiajiri, na azma hiyo itafanikiwa zaidi endapo tutaendelea kuwekeza katika vyuo vya VETA,” amesema Qwaray.

Amefafanua kuwa vijana wanaohitimu elimu ya sekondari au vyuo vikuu wana nafasi ya kujiunga na VETA ili kupata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri badala ya kusubiri ajira za Serikali.

Aidha, amesema mafunzo ya ufundi na stadi mbalimbali yanayotolewa na VETA yana mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa wananchi na kusaidia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

VETA ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza Juni 16, 2026 na kufunguliwa rasmi Juni 17, 2026 na Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa kesho Juni 23, 2026 katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Post a Comment

0 Comments

TMA YAHAMASISHA MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KATIKA MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA