Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MWAKA 2015, serikali ilitayarisha Sera ya Taifa ya Nishati yenye lengo la kutatua changamoto katika mkondo wa kati na wa chini wa shughuli za gesi asilia nchini pamoja na kuwezesha upatikanaji na unafuu wa huduma endelevu na za kisasa za nishati hiyo.
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan Mei mwaka huu alizindua mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2030.
Kutokana na unafuu wa matumizi ya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas CNG),kwenye magari ambapo ujenzi wa vituo vya kujaza gesi hiyo unaendelea kwa kushirikisha pia Sekta Binafsi katika Jiji la Dar es Salaam
Watumiaji wa gesi ya CNG ambao ni madereva bajaji wanaofanya shughuli zao za Usafirishaji katika Jiji la Dar es Salaam wanazungumzia umuhimu wa gesi hiyo katika kuongeza kipato.
Kimweri Ramadhani anayejulikana kama 'Chifu' ni mmiliki wa bajaji ambaye maskani ya kijiwe chake kipo Kariakoo Mtaa wa Narung'ombe anaeleza kuwa awali alikuwa akitumia bajaji ya mafuta ambapo changamoto aliyokuwa akiipata ni kutokukidhi mahitaji yake kwa kipato alichokuwa akikipata kutokana na kutumia fedha nyingi kujaza mafuta hayo huku akisema kwa sasa amenunua bajiji ambayo tayari inatumika mfumo wa CNG.
FAIDA YA CNG
Chifu anazungumzia faida anayoipata kwa kutumia gesi asilia kwenye bajaji yake anasema kwa sasa anatumia kilo nne ya gesi hiyo ambazo anatumia kwa siku nzima na kupata faida nzuri.
"Natumia gharama ya shilingi 6200 tu kwa siku nzima napata faida kutoka kwenye shilingi 27,000 ya awali wakati natumia mafuta hivyo kwa sasa zaidi ya 20,000 naiokoa kwa kutumia gesi asilia," anasema Chifu.
Mmiliki huyo wa bajaji anasema kwa mwezi anapata zaidi ya 600,000 kutoka kwenye bajeti ya awali alipokuwa akitumia mafuta ya shilingi 27,000 huku akisema alikuwa anaokoa fedha kidogo ambayo haikidhi mahitaji yake.
Anafafanua kuwa hiyo 600,000 ilikuwa inaishia kwenye mafuta alipokuwa na bajaji iliyokuwa ikitumia mafuta hayo.
CHANGAMOTO ZA MAFUTA
Anaeleza kuwa changamoto aliyokuwa akiipata ni kutokukidhi mahitaji yake ya kipato kwa kuwa alikuwa akitumia fedha nyingi kujaza mafuta hayo huku akipata kipato kidogo ambapo kwa sasa amenunua bajiji ambayo tayari inatumika mfumo wa CNG.
Chifu anasema awali alikuwa akitumia tenki zima la mafuta ambapo gharama yake ni shilingi 27,000 kwa siku kutokana na gharama hiyo hata kipato chake kilikuwa hakikidhi mahitaji ya familia.
WITO WAKE KWA VIJANA NA SERIKALI
Anawashauri vijana wenzake wanao endesha bajaji kuingia katika mfumo huo ili kuweza kumudu gharama za maisha yao kutokana na unafua uliopo katika kutumia gesi hiyo ya CNG.
Chifu aiomba serikali, Mamlaka husika kuongeza vituo vya kujazia gesi hiyo kutokana na vituo hivyo kuwa vichache.
"Kuna vituo vitatu tu na watumiaji wamekuwa wengi, changamoto tunayoipata ni kukaa muda mrefu kusubiri kujaza gesi, tunaweza kutumia zaidi ya saa mbili.
Naye mwendesha bajaji kutoka mtaa wa Swahili na Narung'ombe Silla Shoo anasema kuwa anatamani kuingia katika mfumo wa bajiji inayotumia gesi hiyo na kwamba kutokana na changamoto ya gharama kubwa ya kubadilisha mfumo huo kutoka katika hali ya kawaida kwenda kuanza kutumia gesi asilia anaona changamoto kwake.
Anaeleza kuwa gharama ya kubadilisha mfumo huo ni shilingi milioni 1.5 hali inayomsababishia kushindwa kumudu gharama hiyo.
Shoo anasema mbali na changamoto ya gharama hiyo foleni kwenye kujaza gesi asilia ni kikwazo kwa waendesha bajaji kwa kuwa wanaotumia mfumo huo wanatumia zaidi ya saa moja kujaza gesi hiyo.
Anaongeza kuwa akienda kujaza mafuta kwenye vituo vya kawaida anatumia muda mchache kujaza mafuta hayo huku akisema anatumia lita 5 kwa siku sawa na shilingi 17,000.
Shoo anasema kutokana na kazi zake lita hizo zinamtosha na kwamba faida anapata.
USHAURI WAKE
Shoo anaishauri Mamlaka husika kuangalia namna ya kupunguza gharama za kufunga mfumo wa gesi asilia kwenye bajaji ili vijana wengi waweze kutumia gesi hiyo.
KAULI YA EWURA
Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),Titus Kaguo anasema kwa sasa vituo vya kujazia gesi ya CNG vingi vipo Dar es Salaam.
"Haiwezi kuchukuliwa gesi hii kupelekwa Dodoma kuna sababu kubwa kwanini mfumo huo unafanyika Dar es Salaam ni kwa kuwa vituo vingi vipo Dar es Salaam, watu wengi wanaulizia waliopo nje ya Dar es Salaam wataipataje gesi hii," anasema.
Anaongeza kuwa mfumo wa gesi hiyo ya CNG hauwezi kujenga kituo kama kilivyo kituo cha mafuta kwamba ichukuliwe kutoka Dar es Salaam ipelekwe Dodoma itakuwa haina thamani kibiashara.
Meneja mawasiliano huyo anasema wanawahamasisha watanzania kuwekeza kwa kufuata maeneo mbalimbali huku akisema CNG matumizi yake watatoka nayo Dar es Salaam watakuja nayo Kibaha, Mlandizi,Chalinze, Morogoro hivyo hivyo hadi inafika Dodoma na kuendeIea hadi Mwanza.
"Na kwenye njia ya Iringa kwenda Mbeya nayo ni hivyo hivyo na hii italeta mafanikio kama watanzania wengi watahamasika kuwekeza kwenye gesi ya CNG kwa kujenga vituo," anasema Kaguo.
Kaguo anaeleza kuwa EWURA inahamasisha na kwamba mtu akiwa Dodoma apeleke gari yake Dar es Salaam ikabadilishwe mfumo na ubadilishaji wake unafanyika Dar es Salaam.
Anasema wanahamasisha watanzania kubadilisha magari yao ili yawe na mifumo yote miwili ya mafuta na ya gesi hiyo ya CNG na kwamba mwitikio ni mkubwa ambapo gari zilizobadilishwa ni nyingi kwa kiwango ambacho EWURA haikutarajia na vituo vinavyotoa huduma vimaeongezeka.
VITUO VYA CNG
Akizungumzia vituo vinavyoa huduma ya gesi asilia anaeleza kuwa jumla vituo vitano vimeshajengwa hadi sasa, dangote ana viwili, Mkuranga na Mtwara viwili na Dar es Salaam vipo vitatu na kuna watu wanaendelea kuomba leseni kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo.
" Tumekaa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), tukakubaliana kurekebisha taratibu za viwango (Standard), kwamba kituo chochote cha mafuta kilichopo hapa nchini mtu anaweza kuwa na kituo cha mafuta na akajenga cha CNG hapo hapo," anaeleza Kaguo.
Anaongeza kuwa utaratibu huo unaruhusiwa na TBS imesharuhusu kwa mujibu wa viwango huku akisema wanaendelea kuhamasisha watanzania kuingia kwenye biashara hiyo.
Meneja wa mawasiliano huyo anaeleza kuwa moja ya kampeni ya kuhamasisha matumizi safi vya nishati ambayo inaongozwa na Rais Dk.Samia suluhu Hassan ni matumizi ya gesi hiyo kwa kuwa haitoi moshi hivyo watakuwa wanatumza mazingira.
"Kampeni ya nishati safi inaenda hadi kwenye nishati aina ya mafuta na uhamasishaji huo, EWURA tutaendelea kuhamasisha watanzania waendelee kuwekeza na kurekebisha magari yao,"; anasema Kaguo.
Anafafanua kuwa mtu akiwa na gesi ya CNG ya shilingi 17,000 hadi 20,000 ambayo ni mtingi wa kilo11 kwa gari aina ya IST inaweza kutoka Dar es Salaam ikafika Morogoro na ikarudi hadi Chalinze huku akisema wakati mafuta ya 20,000 ni sawa na lita sita tofauti ni kubwa.
Anasema bei za mafuta zinaendelea kupanda hivyo watanzania wachangamkie gesi hiyo.
Aidha anawasisitiza watanzania kuwekeza kwenye biashara hiyo kwa kuwa inalipa huku wakiisaidia serikali katika mpango wake ule wa nishati safi.
0 Comments