Na Asha Mwakyonde,Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imepongezwa kwa kuboresha huduma za uwasilishwaji wa taarifa za mamalaka za maji ambazo zinatoa fursa za kuongeza takwimu zaidi kuhusu usafi wa mazingira.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma Agosti 20,2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu),William Lukuvi wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko katika ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Usafi wa Mazingira ambalo limeandaliwa na EWURA na kuwakutanisha wadau wa usafi wa mazingira lenye Kauli mbiu isemayo "Mipango Jumuishi ya Usafi wa Mazingira kwa Afya Bora".
Waziri Lukuvi amesema kuwa takwimu hizo zitasaidia katika mpango wa maendeleo kwenye Sekta ya maji safi ja mazingira.
Amesema kuwa anatambua kongamano hilo limeenda sambamba na uzinduzi wa Muogonzo wa Usimamizi wa Huduma za maji taka na tope kinyesi uliotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili pamoja na mfumo ulioboreshwa wa uwasilishaji wa EWURA.
"Naipongeza EWURA kwa kuufanya muuongozo huu kwa lugha ya Kiswahili unalenga kuziongoza mamalaka za maji safi, usafi wa mazingira katika kutoa huduma zikiwamo za Usimamizi wa tope kinyesi kwa wananchi walio nje ya mtandao wa maji taka," ameleza.
Amefafanua kuwa muongozo wa usimamizi wa topetaka na kinyesi pamoja na mamalaka za maji unawalenga wadau wengine kama mamalaka za serikali za mitaa, Sekta binafisi zinazotoa huduma hizo kwenye maeneo yasiyo na mtandao wa maji taka.
Waziri Lukuvi ameongeza kuwa muongozo huo unatia faraja kuona unakwenda kutekeleza mipango ya serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha inatekeleza miradi ya kimkakati ya kujenga mfumo wa uondoaji maji taka katika miji yote ya makao makuu ya mikoa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile ameeleza kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuhakikisha inaimarisha afya za watu wake ikiwamo suala la upatikanaji wa maji safi kwa wingi.
Ameeleza kuwa usafi wa mazingira ni afya na kwamba tathimini walioifanya kwa kuzingatia tafiti walizozifanya katika Karne ya 19 ilithibitika pasipo na shaka pale watu wanapo kaa kwenye mazingira hayo mazuri afya zao zinakuwa imara na wanazidi kujikinga na magonjwa.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa serikali imekuwa ikihimiza suala la matumizi ya nishati safi kwa lengo la kuimarisha masuala ya afya kwa watu wake.
"Tumekusanyika hapa mchana wa leo kwa lengo la kutafakari mikakati ya pamoja ya kuboresha masuala ya usafi wa mazingira," ameeleza Dk.Andilile.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA Victoria Elangwa amesema kuwa Bodi hiyo inaunga mkono masuala hayo ya mazingira pamoja na kongamano hilo na kwamba kesho kutakuwa na kikao kazi ambapo wataalam watachakata na kujadili namna mbalimbali na bora ya kutunza mazingira katika muktadha wa usalama na usafi wa maji.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Omar Ali Yussuf ameeleza kuwa kongamano hilo ni faraja kwao huku akiahidi nao watachukua yote yatakayo jadiliwa na wataalam pamoja napendekezo ili kuhakikisha yote ya Muungano wa Tanzania yapo salama kwa upande wa Bara na Visiwani.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya maji safi na mazingira Anna Lupembe ameipongeza EWURA kwa kuona umuhimu wa kongamano hilo kwa ajili ya Taifa zima kwa kuhakikisha, kusimamia mazingira.
Aidha ametoa wito kuwa kongamano hilo lisiishie hapo bali waende kwenye maeneo kwa ajili ya kufanya kazi kwa uhalisia, vitendo.
0 Comments