Na Asha Mwakyonde DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kufanya Utafiti unaohusiana na uzalishaji wa mnyama kazi punda, kufanya maboresho kwenye mtaala wa mafunzo kwenye vyuo vya mifugo.
Hayo yamesemwa leo Septemba 25,2024 jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Uvuvi wa Mifugo anayeshughulikia Ustawi wa Wanyama Dk.Annette Kitambi wakati akiwasilisha mada katika mdahalo wa siku mbili wa wadau wa mnyama kazi punda ambao unajadili tafiti ambazo zimefanywa na wataalam waliopewa kazi na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Inades-Formation Tanzania (IF TZ), inayofadhiliwa na Brooke East Africa baada ya serikali kusitisha uchinjaji wa mnyama huyo hapa nchini.
Amesema matarajio mengine ni kuanzisha ufugaji wa mnyama kazi punda kwenye mashamba ya mifugo ya wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau ustawi wa mnyama huyu.
"Oktoba 1, 2021 katazo la serikali lilikataza nyama ya punda na ngazi na kwa sasa mbwa na paka wamekatazwa wasiliwe," amesema Mkurugenzi huyu.
Akizungumzia hali ya ustawi wa mnyama huyo amesema mara nyingi hubebeshwa mzigo mkubwa kuliko anachostahili.
"Hatua zilizochukuliwa kwa ajili ya uboreshaji wa mnyama huyu ni kutoa elimu ya ustawi kwenye vyombo vya habari, uteuzi wa Bodi ya kushauri Waziri masuala ya ustawi," amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa IF TZ Mbarwa Kivuyo, amefafanua kuwa walipeleka wataalam katika maeneo matatu ambayo ni kuangalia hali ikoje tangu serikali ilivyopiga marufuku biashara ya uchinjaji wa mnyama kazi punda.
"Leo na kesho wataalam wanatoa taarifa zao baada ya kufanya utafiti uchinjaji wa mnyama kazi punda hapa nchin, hali ikoje,sheria inasema kila mtafiti atawasikisha taarifa yake," ameeleza Kivuyo.
Kwa upande wake Afisa Uchechemuzi na Mambo ya Nje kutoka Shirika la Brooke East Africa Samwel Theuri amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika kukataza biashara ya nyama ya mnyama kazi Punda na bidhaa yake ya ngozi pamoja na kufanya sensa ya mnyama huyo.
" Tutazidi kushirikiana nanyi katika kuendeIeza mradi huu wa kumlinda na kumtunza mnyama kazi punda," ameeleza Theuri.
Daktari wa Mifugo kutoka sekta binafisi Dk. Bedan Masuruli akiwasilisha taarifa ya tathimini ya hali ya biashara ya mnyama kazi punda kuhusu tamko la kupigwa marufuku nchini uchinjaji wa mnyama huyo ameeleza Usafirishaji wa punda bado unaendelea na kwamba wizara ya mifugo na kwamba wizara hiyo pia inatoa vibali kwa ajili ya kazi nyingine.
"Mnyama kazi Punda wanaosafirishwa ni wale wanaokwenda mkoani Geita ambapo awali soko halikwepo katika Mkoa huu na hakuna Sheria inayomkataza mtu asile Punda," amesema.
Ameongeza kuwa usafirishwaji wa punda na vibali vinaendelea kutolewa ili kupeleka mifugo hiyo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa hususan Shinyanga na Geita na kwa kiasi fulani Mkoa wa Singida.
Daktari Masuruli ameeleza kuwa uchinjaji wa punda hufanyika kila siku kwa wastani wa punda mmoja kwa siku na hadi punda kumi siku ya soko.
Naye daktari Mstaafu wa mifugo Mohamed Bahari amesema Tanzania ina Sera ya Taifa ya Mifugo ambapo mwaka 2006 ambayo ilipitiwa upya huku mchakato wa mapitio ukikaribia kumalizika ili kukumbatia misukumo mipya kama vile kuhimili mabadiliko ya tabianchi, kilimo bora na ufugaji endelevu.
Dk. Bahari ameeleza uelewa mdogo na ukosefu wa taratibu za utekelezaji utafiti umebaini kuwa ni mapungufu makubwa yanayochangia kukosekana kwa meno kwa Sheria na taasisi yake iliyoanzishwa Baraza la Ushauri la Ustawi wa Wanyama pamoja na kuwatenganisha wahusika hai kati ya Wizara ya Kisekta ya Mlinzi inayohusika na ustawi wa wanyama Mkoa.
0 Comments