SAFARI YA EWURA KATIKA KUBORESHA HUDUMA KWA WATEJA


📍Kutoka Ofisini hadi Kidijitali

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

KATIKA dunia inayobadilika kwa kasi, huduma kwa wateja si tu jukumu la kisheria, bali ni msingi wa uaminifu na maendeleo ya taasisi. Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025 inakuja kama jukwaa mahsusi la kutafakari, kusherehekea na kuboresha uhusiano kati ya watoa huduma na wananchi.

Kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), taasisi inayosimamia sekta nyeti za nishati na maji, wiki hii si tukio la kawaida bali ni fursa ya kuonesha dhamira yake ya dhati ya kusikiliza, kuhudumia, na kujenga mahusiano imara na wadau wake.

Chini ya kaulimbiu ya mwaka huu,"Mission Possible" Dhamira Inayowezekana,EWURA inaangazia umuhimu wa kuimarisha mifumo ya mawasiliano, kuongeza uwazi katika maamuzi na kuhakikisha kuwa sauti ya mwananchi inasikika na kuchukuliwa hatua.

Katika makala haya, tunaangazia jinsi EWURA inavyobadilisha huduma kwa wateja kutoka kuwa mchakato wa kawaida hadi kuwa chombo cha mageuzi ya kijamii na kiuchumi.

MAJUKUMU YA EWURA

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, anabainisha kuwa taasisi hiyo inahusika na udhibiti wa masuala ya kiuchumi na kiufundi katika sekta ya nishati  ikijumuisha mafuta, gesi asilia, na umeme  pamoja na sekta ya huduma ya maji na usafi wa mazingira.

Dk.Andilile anawakaribisha wadau na wateja wote kushiriki katika maadhimisho ya wiki hii muhimu, akisisitiza kuwa kwa EWURA, wateja wao ni pamoja na watoa huduma pamoja na wananchi wanaotumia huduma hizo.

Anasisitiza kuwa wateja ni kiini cha upatikanaji na utoaji wa huduma bora, kwani wao ndio kipimo cha mwisho cha mafanikio ya EWURA kama msimamizi wa huduma na pia kwa watoa huduma waliopo chini ya uangalizi wao.

“Tunapoadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, tunapata nafasi ya kutafakari kwa pamoja namna tunavyotekeleza majukumu yetu katika kuwahudumia wananchi kwa ufanisi. Leo hii huduma nyingi za EWURA zinapatikana kidijitali," amesema Dk. Andilile.

HUDUMA KIDIJITALI KWA UFANISI 

Anaeleza kuwa EWURA imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa maombi ya leseni (LOIS – Licensing Online Information System), unaomwezesha mteja kupata huduma bila kufika ofisini huku akisema mteja hujaza taarifa zake mtandaoni na kupelekewa leseni endapo masharti yote ya kisheria yametimizwa.

Mkurugenzi Mkuu huyo anaeleza kuwa kwa upande wa watumiaji wa huduma, EWURA imeanzisha  mfumo wa e-LUC, unaopatikana kupitia simu za mkononi, ambao unamwezesha mteja kutoa taarifa na maoni kuhusu huduma za umeme, mafuta, gesi, na maji.

 “Mfumo huu unahakikisha tunapata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa mikataba ya huduma kwa wateja. Ni njia ya uwazi na ushirikishwaji wa umma," anabainisha Dk. Andilile.

ELIMU KWA UMMA NA UWAJIBIKAJI WA SHERIA 

Anaeleza kuwa kupitia utekelezaji wa kifungu cha 6(e) cha Sheria ya EWURA, Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania, Mamlaka hiyo ina jukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa watoa huduma na walaji, ikiwa ni pamoja na njia za kutatua migogoro na kushughulikia malalamiko.

Akizungumzia Wiki ya Huduma kwa Wateja Kama Kipimo cha Mafanikio Dk. Andilile anasema wiki hii ni muda muafaka kwa taasisi hiyo kutafakari kuhusu utekelezaji wa mkataba wa huduma kwa wateja na kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta tunazozisimamia. Ni jukumu letu kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa kiwango kinachotarajiwa na kwa manufaa ya wananchi," amesema.

Ameongeza  kuwa EWURA itaendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia na kusikiliza sauti za wananchi ili kuhakikisha ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa yanaimarika kupitia huduma bora na zenye kuleta tija.

Post a Comment

0 Comments

MATIVILA AAGIZA MKANDARASI KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA