WAFANYABIASHARA WA MISITU WAENDA MAHAKAMANI KUPINGA KANUNI MPYA


Na Mwandishi wetu, DODOMA 

WAFANYABIASHARA wanaojihusisha na biashara ya mazao ya misitu wamefungua shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu Dodoma wakiishtaki Serikali, wakipinga kanuni ndogo mpya za uendeshaji wa uvunaji wa mazao ya misitu ambazo wanasema utekelezwaji wake unawasababishia hasara kubwa katika biashara zao.

Kupitia kwa mwanasheria wao, Mohamed Tibanyendera, wafanyabiashara hao wamefungua maombi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, wakipinga kanuni hizo zilizochapishwa kwenye Tangazo la Serikali Namba 132 la Februari 22, 2025, ambalo linarekebisha Kanuni Namba 153 ya mwaka 2004.

Maombi hayo yalitarajiwa kuanza kusikilizwa leo Disemba15, 2025 mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Iman Aboud, hata hivyo yaliahirishwa hadi Desemba 18, 2025 na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma, Mwajabu Mvungi, kutokana na kutokuwepo kwa Jaji Aboud mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma, Tibanyendera alisema wafanyabiashara hao wanapinga kanuni hizo kwa madai kuwa taratibu za kisheria za marekebisho ya sheria hazikufuatwa, licha ya wao kuwa wadau wakuu wa sekta ya misitu wakiwemo wafanyabiashara, wavunaji na wasafirishaji wa mazao ya misitu.

Amesema kuwa matokeo ya kutofuatwa kwa taratibu hizo ni mamlaka inayosimamia masuala ya misitu nchini, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuanza kutekeleza kanuni hizo kwa namna ambayo wafanyabiashara wanaona inawabagua na kuwanyima haki zao za kibiashara, hususan katika suala la tozo ya royalty na kiwango cha mazao wanayoruhusiwa kuvuna.

Kwa mujibu wa Tibanyendera, wafanyabiashara hao hulazimika kulipia mti mzima, lakini wanaporuhusiwa kuvuna, huambiwa wachukue gogo pekee, huku wakizuiwa kuchukua matawi, majani na sehemu nyingine za mti huo, jambo linaloongeza hasara kwa kuwa tayari wamegharamia mti mzima.

 “Mfadhili analipia mti mzima kuanzia mizizi, shina, matawi na majani, lakini anapoenda kuvuna anaambiwa achukue gogo pekee. Sehemu zinazobaki zinaelezwa kuwa ni mali ya Serikali, hali ambayo ni dhuluma kwa mlipaji,” amesema Tibanyendera.

Ameongeza kuwa wafanyabiashara hao wanaomba Mahakama itamke kuwa kanuni hizo ni batili kwa kuwa zinakinzana na taratibu za utungwaji wa sheria, sambamba na kuagiza mamlaka husika kuzingatia haki zao na kufuata taratibu zote za kisheria kabla ya kutekeleza kanuni zinazogusa shughuli zao.

Ameeleza kuwa licha ya wafanyabiashara kulipa fedha nyingi kwa ajili ya vibali na tozo mbalimbali, mara nyingi hukumbana na mabadiliko ya ghafla ya taratibu wanapojaribu kusafirisha au kutumia mazao waliyolipia, hali inayodaiwa kuathiri kwa kiasi kikubwa uendeshaji wa biashara zao.

Post a Comment

0 Comments

SERIKALI YAHIMIZA MAADILI NA UZALENDO