Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MFUMO wa haki jinai nchini umeendelea kuimarika kwa kasi kupitia maboresho ya kimkakati yanayolenga kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa mashtaka, kulinda haki za binadamu na kujenga imani ya wananchi kwa vyombo vya sheria.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera ameeleza hayo bungeni jijini hapa leo Aprili 24,2026 wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema Wizara kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kutekeleza jukumu la kuendesha kesi za jinai katika ngazi mbalimbali za mahakama nchini.
Waziri huyo amesema sambamba na hilo, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kutenganisha shughuli za mashtaka na upelelezi ili kuhakikisha taasisi hizo zinafanya kazi kwa uhuru, uwajibikaji na weledi zaidi, hatua inayolenga kuimarisha utawala wa sheria na kuboresha utoaji wa haki jinai.
Dk.Homera amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya kesi za jinai 17,612 ziliendeshwa katika Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi, ambapo kesi 14,522 sawa na asilimia 82 zilihitimishwa na kwamba kati ya hizo, kesi 10,640 sawa na asilimia 73 zilimalizika kwa watuhumiwa kutiwa hatiani.
Ameongeza kuwa katika Mahakama za Watoto, kesi 377 ziliendeshwa na kati ya hizo asilimia 89.1 zilihitimishwa, huku asilimia 83.3 ya kesi zilizohitimishwa zikiishia kwa watuhumiwa kutiwa hatiani.
Kwa upande wa Mahakama Kuu, amesema kesi 2,491 ziliendeshwa katika kanda mbalimbali, huku rufaa na maombi 389 ya Mkurugenzi wa Mashtaka yakisikilizwa, idadi inayodhihirisha ongezeko la shughuli za kimashtaka katika ngazi za juu za mahakama.
Aidha, ameeleza kuwa katika Mahakama ya Rufani, jumla ya rufaa na maombi 1,280 yalisikilizwa, ambapo sehemu kubwa ilikuwa dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, jambo linaloonesha uendelevu wa mchakato wa haki katika ngazi ya juu zaidi ya mahakama.
Dk. Homera amesema Serikali pia imeendelea na zoezi la kutaifisha mali zitokanazo na uhalifu, ambapo nyumba 10, viwanja 16, pamoja na fedha taslimu na hati fungani zenye thamani ya mamia ya milioni ya shilingi zilikamatwa na kuwa mali ya Serikali.
"Hatua hii inalenga kudhibiti uhalifu na kuondoa motisha ya watu kujihusisha na vitendo vya uhalifu, akibainisha kuwa uhalifu haulipi," amesisitiza.
Akizungumzia kuimarisha haki kwa vitendo, amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefanya ukaguzi katika magereza 94 na vituo vya polisi 483, ambapo mahabusi 918 waliachiwa huru kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.
Ameongeza kuwa ukaguzi maalum pia ulifanyika kwa watoto waliokinzana na sheria katika mikoa mbalimbali, ambapo majalada 59 yalifanyiwa mapitio na kusaidia kuharakisha upelelezi na usikilizwaji wa kesi hizo.
Waziri huyo amebainisha kuwa Serikali imeendelea kusogeza huduma za mashtaka karibu na wananchi kwa kufungua ofisi mpya za wilaya 10, hatua iliyofikisha jumla ya ofisi 118 kati ya wilaya 139 nchini.
Amefanunua kuwa Mawakili wa Serikali 78 wameajiriwa ili kuimarisha utendaji kazi katika ngazi za mikoa na wilaya na kupunguza upungufu wa watumishi.
Dk. Homera amesema maboresho hayo yanaendelea kuleta matokeo chanya katika sekta ya sheria kwa kuongeza ufanisi, kupunguza msongamano wa mahabusi na kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati na kwa usawa kwa wananchi wote.
.jpg)
0 Comments