Na Asha Mwakyonde, DODOMA
USHIRIKIANO wa muda mrefu kati ya Bunge Bonanza na Benki ya CRDB umeendelea kuzaa matunda, huku wadau wakieleza kuwa mchango wa benki hiyo umeifanya shughuli ya michezo kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha afya, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa washiriki mbalimbali.
Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, amesema udhamini wa CRDB Bank kwa miaka mitano mfululizo umechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji na mafanikio ya bonanza hilo, ambalo limeendelea kuvutia ushiriki wa wabunge, watumishi wa Bunge pamoja na wadau kutoka sekta mbalimbali.
Akizungumza leo 20,2026 katika Bunge Grand Bonanza lililofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Sanga amesema ushirikiano huo umeiwezesha shughuli hiyo kuendelea kupanuka mwaka hadi mwaka na kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya washiriki.
Amesema mafanikio yanayoonekana leo ni matokeo ya mchango wa wadau mbalimbali wanaoendelea kuunga mkono bonanza hilo, huku CRDB Bank ikibaki kuwa mmoja wa washirika wakuu wanaochangia kufanikisha malengo yake.
“Tunafurahia kuona Bunge Bonanza likikua na kupata ushiriki mkubwa zaidi kila mwaka. Mafanikio haya yanatokana na ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau wetu, hususan CRDB Bank ambayo imeendelea kuwa nasi kwa miaka mitano mfululizo,” amesema Sanga.
Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Abdulmajid Nsekela, pamoja na menejimenti ya benki hiyo kwa kuendelea kuunga mkono shughuli zinazochochea ustawi wa jamii na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika michezo.
Sanga ameeleza kuwa mbali na huduma zake za kifedha, CRDB imeendelea kujitokeza katika kusaidia programu mbalimbali za maendeleo ya jamii, hatua inayochangia ustawi wa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Aidha, ameipongeza benki hiyo kwa juhudi zake za kupanua huduma na shughuli zake ndani na nje ya Tanzania, akieleza kuwa hatua hiyo inasaidia kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Sanga amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi una nafasi kubwa katika kuharakisha maendeleo na kuleta manufaa kwa wananchi, huku akizitaka taasisi mbalimbali kuendelea kushirikiana katika kutekeleza mipango yenye tija kwa jamii.

0 Comments