TBA YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA KUPITIA UBUNIFU NA TEKNOLOJIA


 Na Asha Mwakyonde, DODOMA

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeeleza kuwa unaendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na taasisi za umma kupitia uwekezaji wa miradi mbalimbali, matumizi ya mifumo ya kidijitali na maendeleo ya rasilimali watu, hatua zinazolenga kuongeza ufanisi na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wakati.

Akizungumza leo Juni 19, 2026 katika Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Meneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa TBA, Lumuli Mwangosi, amesema taasisi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia uwajibikaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Amesema ushiriki wa TBA katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo, ikiwemo ushauri wa kitaalamu katika ujenzi wa majengo ya serikali, upangishaji wa nyumba za watumishi wa umma pamoja na usimamizi wa ofisi za serikali.

Mwangosi amebainisha kuwa TBA kwa sasa inaendelea kutekeleza miradi kadhaa ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mali za serikali na kuboresha huduma kwa wananchi.

“Tunatumia fursa hii kuwafikia wananchi na kuwapa taarifa kuhusu majukumu yetu pamoja na miradi mbalimbali ya uwekezaji tunayoitekeleza. Tunawakaribisha kutembelea banda letu ili kupata maelezo ya kina kuhusu huduma zetu,” amesema.

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu ya Wiki ya Utumishi wa Umma inayosema ‘Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu’, alisema uwajibikaji wa watumishi ni msingi muhimu wa mafanikio ya taasisi yoyote ya umma.

Ameeleza kuwa TBA ina wataalamu wa kada mbalimbali wanaoshirikiana kutekeleza majukumu ya taasisi, wakiwemo wahandisi, wataalamu wa utawala, makatibu, madereva na watumishi wengine, ambapo mchango wa kila mmoja ni muhimu katika kufanikisha malengo ya taasisi.

Mwangosi amesema TBA imeendelea kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia kwa kutumia mifumo mbalimbali ya kidijitali inayosimamiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ikiwemo mifumo ya Watumishi, Mrejesho, Msawazo, Mikopo na Mfumo wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma (PEPMIS).

Kwa mujibu wake, matumizi ya mifumo hiyo yamechangia kuimarika kwa uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za watumishi wa umma.

Ameongeza mfumo wa PEPMIS umewezesha watumishi kupimwa kwa kuzingatia malengo waliyojiwekea, jambo ambalo limeongeza tija na kuimarisha utendaji kazi katika taasisi.


Aidha, ameeleza TBA imeweka mkazo katika kuwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu yanayolenga kuwawezesha kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa watumishi wa kada zote ili kuongeza ujuzi, kuimarisha taaluma na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mwangosi amesisitiza kuwa TBA itaendelea kuwekeza katika teknolojia na maendeleo ya rasilimali watu ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa za kisasa, zenye ufanisi na zinazokidhi matarajio ya wananchi.

Post a Comment

0 Comments

WANAFUNZI KUNUFAIKA NA ELIMU YA ULINZI WA MLAJI KUPITIA KLABU ZA FCC