Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imesema imejizatiti kuimarisha ubora na kasi ya huduma za uchunguzi wa kisayansi kwa kutumia mifumo ya kidijitali na maabara zenye viwango vya kimataifa, hatua inayoongeza ufanisi katika uchunguzi wa makosa ya jinai pamoja na uchambuzi wa sampuli mbalimbali zinazohusu afya na usalama wa wananchi.
Hayo yameelezwa leo Julai 5,2026 na Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai wa GCLA, David Elias,katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba,ameasema maabara za mamlaka hiyo zinafanya uchunguzi wa aina mbalimbali za sampuli, zikiwemo za vyakula, maji, vinywaji, dawa na bidhaa nyingine zinazotumiwa na binadamu kwa lengo la kulinda afya na usalama wa wananchi.
Amesema maabara za GCLA zimeidhinishwa kwa viwango vya kimataifa, hali inayofanya matokeo ya uchunguzi yanayotolewa kutambulika na kukubalika ndani na nje ya Tanzania.
Mkurugenzi huyo akizungumzia uchunguzi wa makosa ya jinai, Elias amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika vifaa vya kisasa pamoja na teknolojia za kisayansi zinazoongeza ufanisi na usahihi wa uchunguzi.
Amefafanua kuwa pale afisa anayefika eneo la tukio anapokuwa na shaka kuhusu sampuli aliyoikusanya, anaweza kuiwasilisha GCLA kwa uchunguzi wa kina, ambapo mfumo wa kidijitali huwezesha kufuatilia hatua zote za uchunguzi kuanzia sampuli inapopokelewa maabara hadi matokeo yanapotolewa.
"Mfumo huu unamwezesha mhusika kupata taarifa kwa wakati kuhusu maendeleo ya uchunguzi, jambo linaloongeza uwazi, uwajibikaji na kuharakisha utatuzi wa mashauri mbalimbali, hususan ya jinai," amesema.
Aidha, amesema GCLA inaendelea kutumia teknolojia za kisasa za uchunguzi wa kisayansi zinazosaidia kubaini wahusika wa uhalifu kwa usahihi mkubwa kupitia ushahidi wa kisayansi unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wa Elias, matumizi ya teknolojia hizo yanachangia kuhakikisha wahalifu hawakwepi mkono wa sheria kutokana na uwepo wa ushahidi wenye ubora na unaoaminika.
Amesisitiza kuwa GCLA itaendelea kuboresha huduma zake kwa kuzingatia viwango vya kimataifa ili kuwahakikishia wananchi, wawekezaji na wadau wengine kuwa matokeo ya uchunguzi yanayotolewa yanaaminika na yanatambulika ndani na nje ya nchi.
"Watanzania waendelee kuwa na imani na huduma zetu, kwani maabara zetu zimejengwa katika misingi ya taaluma, teknolojia na viwango vya kimataifa vinavyohakikisha kila uchunguzi unafanyika kwa usahihi na uadilifu," amesema Elias.
Aidha amewakaribisha watanzania kutembelea banda la Mamlaka hiyo Sabasaba ili kuweza kupata elimu kuhusu masula mbalimbali ya makosa Jinai.



0 Comments