Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, ameshuhudia vijana waliomaliza kidato cha nne na kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano katika tahasusi mbalimbali, ambapo baadhi yao wamekuwa na wasiwasi kuhusu uchaguzi huo wakidhani huenda haukuwa sahihi licha ya wao wenyewe kuuchagua awali.
Amesema moja ya taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo, ni pamoja na Ofisi wa Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), zimekuwa zikitoa huduma muhimu kwa wananchi hususan wanafunzi na wazazi wanaopata changamoto katika uchaguzi wa tahasusi.
Prof. Kabudi ameyasema hayo Julai 4,2026 alipotembelea banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF),amesema kupitia wataalamu waliopo katika banda hilo, vijana hao wamekuwa wakipatiwa ushauri nasaha na mwongozo unaowasaidia kuelewa vizuri tahasusi walizopangiwa na namna ya kufanya mabadiliko pale inapobidi ili ziendane na uwezo wao kitaaluma.
Amewahimiza wananchi kutembelea banda la Ofisi hiyo katika maonesho hayo ili kupata huduma na ushauri kuhusu masuala mbalimbali ya kiserikali.
Prof.Kabudi ameongeza kuwa kupitia banda hilo, wananchi wanapata fursa ya kusikiliza na kuwasilisha changamoto zao ambazo zinapokelewa na kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za Umma.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo kwa Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano kutoka TAMISEMI, Roida Andusamile amesema kuwa banda hilo limekuwa likipokea wanafunzi wengi waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano na kuwapatia elimu katika maonesho hayo.
Amefafanua wazazi pamoja na wanafunzi hao hupatiwa elimu kuhusu mfumo wa upangaji wa tahasusi na hivyo kuondoka wakiwa wamepata uelewa zaidi kuhusu hatua hiyo muhimu ya elimu.


0 Comments