TPDC YALEZA MAFANIKIO NA MIPANGO YA KUONGEZA MATUMIZI YA GESI ASILIA

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM 

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeeleza kuwa linaendelea kupanua matumizi ya gesi asilia nchini, likilenga zaidi sekta ya nishati ya kupikia majumbani kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wengi wanapata nishati safi, salama na yenye gharama nafuu.

Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Masoko wa TPDC, Neema Cleophace, alisema shirika hilo linaendelea kusogeza huduma za gesi asilia karibu zaidi na wananchi ili kuongeza matumizi yake katika sekta mbalimbali.

Amefafanua kuwa gesi asilia inayozalishwa nchini inapatikana katika mikoa ya Mtwara na Lindi, na inatumika katika maeneo mbalimbali yakiwemo majumbani, usafiri wa magari, viwandani pamoja na uzalishaji wa umeme.

Amesema takribani asilimia 70 ya gesi asilia inayozalishwa nchini hutumika katika kuzalisha umeme, huku TPDC ikiwa tayari imeunganisha zaidi ya nyumba 2,500 kutumia gesi hiyo kwa matumizi ya majumbani.

Akizungumzia sekta ya usafiri, Cleophace amesema matumizi ya gesi asilia yanaendelea kuongezeka, ambapo zaidi ya magari 5,000 tayari yameanza kutumia nishati hiyo kupitia vituo zaidi ya 18 vya kujazia gesi asilia vilivyopo nchini.

Aidha, amebainisha kuwa zaidi ya viwanda 59 nchini vinatumia gesi asilia katika shughuli zao za uzalishaji, hatua inayosaidia kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.

Akizungumzia mipango ya mwaka wa fedha huu, Cleophace ameeleza kuwa TPDC imejipanga kuongeza kasi ya uunganishaji wa nyumba mpya zitakazotumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia.

“Kwa Dar es Salaam tunatarajia kuunganisha zaidi ya nyumba 1,000. Pia tuna mpango wa kuunganisha zaidi ya nyumba 800 Mkuranga na nyingine 800 katika Mkoa wa Mtwara,” amesema.

Amewataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya Sabasaba kutembelea banda la TPDC ili kupata elimu kuhusu shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo pamoja na kujifunza faida za matumizi ya gesi asilia katika maisha ya kila siku.

Cleophace amesisitiza kuwa TPDC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha matumizi ya gesi asilia yanaongezeka nchini, hatua itakayochangia upatikanaji wa nishati safi, salama na yenye gharama nafuu kwa wananchi na sekta za uzalishaji.

Post a Comment

0 Comments

TAEC: MAANDALIZI YA UZALISHAJI WA UMEME WA NYUKLIA YAANZA KWA KUZINGATIA USALAMA