SERIKALI YAITAMBUA NBS KWA MCHANGO WAKE KATIKA MAENDELEO YA TAIFA


Na Asha Mwakyonde,DAR ES SALAAM 

NAIBU Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mchango wake katika uzalishaji wa takwimu sahihi na zenye ubora huku akisema taarifa hizo zinaendelea kuwa nguzo muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa.

Akitembelea banda la NBS katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Luswetula amesema ameridhishwa na kazi inayofanywa na taasisi hiyo, hususan katika kuandaa machapisho na taarifa za takwimu zinazotumiwa na Serikali, watunga sera na wadau mbalimbali kufanya maamuzi yenye tija.

Amebainisha kuwa takwimu sahihi ni msingi wa upangaji wa miradi ya maendeleo na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo aliitaka NBS kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia viwango vya kitaaluma.

Kwa upande wake, Meneja wa NBS Mkoa wa Dar es Salaam, David Danda, amesema taasisi hiyo inafarijika kuona viongozi wa Serikali wanatambua na kuthamini juhudi zinazofanywa katika kuboresha huduma za takwimu nchini.

Hata hivyo, Danda alisema bado kuna changamoto ya uelewa kwa baadhi ya wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika tafiti na sensa mbalimbali zinazofanywa na NBS. 

Ameeleza kuwa taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na viongozi na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa umma ili kuongeza ushiriki wa wananchi na kuimarisha ubora wa takwimu zinazozalishwa.

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yalianza Juni 28, 2026, na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026.

Post a Comment

0 Comments

UMMY: TAASISI ZIHAKIKISHE WATU WENYE ULEMAVU WANASHIRIKISHWA KIKAMILIFU