Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
Tume ya Ushindani (FCC) imewahimiza wananchi, wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo usajili wa mikataba, upokeaji na usikilizaji wa malalamiko pamoja na elimu kuhusu bidhaa bandia na ushindani wa haki sokoni.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa FCC, Roberta Feruzi, amesema taasisi hiyo imejipanga kutoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi wote watakaotembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara, sambamba na kutoa elimu kuhusu majukumu ya FCC.
Amesema maonesho hayo yanawakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za biashara, hivyo FCC imeutumia mkusanyiko huo kuwafikia makundi tofauti ya wafanyabiashara na wajasiriamali kwa kuwapatia elimu itakayowasaidia kufanya biashara kwa kuzingatia sheria na kanuni za ushindani.
"Tunatoa semina mbalimbali kwa wafanyabiashara kila siku katika kipindi chote cha maonesho. Hatuishii kutoa huduma ndani ya banda pekee, bali pia tunawafuata wafanyabiashara walipo ili kuhakikisha elimu inawafikia wengi zaidi," amesema Feruzi.
Ameeleza kuwa kampeni ya utoaji wa elimu inalenga kuongeza uelewa kuhusu ushindani wa haki, kuwalinda walaji na kuwajengea uwezo wafanyabiashara ili waendeshe shughuli zao kwa kuzingatia sheria za ushindani.
Aidha, amesema FCC inaendelea kutekeleza maono ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuchangia ujenzi wa uchumi jumuishi kupitia mazingira yanayowezesha biashara kukua na kushindana kwa haki.
Feruzi amewakaribisha wananchi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kutembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupata huduma na elimu kutoka FCC pamoja na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo.


0 Comments