TMDA YATOA WITO WA KUFICHUA WANAOUZA DAWA BANDIA NA ZISIZOSAJILIWA

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa bandia, vifaa tiba bandia na bidhaa za afya ambazo hazijasajiliwa kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika, ikisisitiza kuwa ushiriki wa jamii ni nguzo muhimu katika kulinda afya za Watanzania.

Hayo yamesemwa leo Julai 6,2026 na Meneja wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma kutoka TMDA, Gaudensia Simwanza, amesema udhibiti wa dawa na bidhaa za afya si jukumu la TMDA pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi, hivyo jamii inapaswa kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na uuzaji au usambazaji wa dawa na vifaa tiba visivyo na ubora, bandia au ambavyo havijasajiliwa.

"Tunatambua kuwa watu wanaouza bidhaa hizo wanaishi ndani ya jamii. Ndiyo maana tunatoa wito kwa wananchi kuwafichua ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa na afya za wananchi zilindwe," amesema Simwanza.

Amefafanua kuwa TMDA ina Sera ya Kulinda Watoa Taarifa (Whistleblower Policy), inayohakikisha usiri na usalama wa mtu yeyote anayetoa taarifa kuhusu utengenezaji, uuzaji au usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyosimamiwa na mamlaka hiyo, hivyo wananchi hawapaswi kuogopa kutoa taarifa.

Aidha, amesema kufumbia macho uwepo wa dawa bandia, bidhaa zisizo na ubora au ambazo hazijasajiliwa kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji na jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Simwanza, bidhaa ambazo hazijasajiliwa ni hatari kwa sababu ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa na mamlaka, hivyo mtumiaji huwa hajui anachotumia wala athari zinazoweza kujitokeza.

Ameongeza kuwa dawa bandia mara nyingi hazina viambato sahihi vya kutibu ugonjwa husika na yaliyomo ndani yake hayajulikani, jambo linaloweza kusababisha mgonjwa kuchelewa kupona, kuendelea kuugua au kupata matatizo mengine ya kiafya.

Pia amesema matumizi ya dawa hizo hupunguza uwezo wa mtu kufanya kazi na kuzalisha, hivyo kuathiri kipato chake binafsi pamoja na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

"Katika baadhi ya matukio, matumizi ya dawa bandia au zisizosajiliwa yanaweza kusababisha madhara makubwa zaidi, ikiwemo kuhatarisha maisha ya mtumiaji na hata kusababisha kifo," amesema.

Kutokana na hali hiyo, TMDA imewataka wananchi kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya dawa bandia kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaozalisha, kuuza au kusambaza bidhaa hizo, hatua ambayo itasaidia kulinda afya na usalama wa Watanzania.

Post a Comment

0 Comments

WANANCHI ZAIDI YA 1,000 WANUFAIKA NA HUDUMA ZA KISHERIA SABASABA