WANANCHI ZAIDI YA 1,000 WANUFAIKA NA HUDUMA ZA KISHERIA SABASABA

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

WIZARA ya Katiba na Sheria imeendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF),kama jukwaa la kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu ya masuala ya sheria na kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.

Akizungumza Julai 7, 2026 katika maonesho hayo Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Usuluhisho kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili Felix Chakila, alisema lengo la ushiriki wa wizara hiyo ni kutangaza huduma zake pamoja na kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi kuhusu haki na wajibu wao.

Amesema tangu wizara ilipoanza kutoa huduma katika maonesho hayo Juni 28 mwaka huu 2026, tayari imewahudumia takribani wananchi 1300 waliowasilisha changamoto mbalimbali za kisheria na kupata ushauri pamoja na mwongozo wa namna ya kuzitatua.

Chakila amesema miongoni mwa masuala yanayowasilishwa kwa wingi ni migogoro ya mirathi, kesi za jinai, changamoto zinazohusisha taasisi za Serikali pamoja na migogoro ya ardhi.

Amefafanua kuwa baadhi ya wananchi wamepatiwa ushauri wa moja kwa moja, huku wengine wakielekezwa kwenye mamlaka husika zenye uwezo wa kushughulikia na kutatua changamoto zao kwa mujibu wa sheria.

Aidha, amewahimiza wananchi kutumia siku zilizobaki za maonesho hayo kutembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata elimu ya kisheria, ushauri na huduma mbalimbali zitakazowasaidia kutatua changamoto zao kwa njia sahihi za kisheria.

Wakili Chakila ameeleza kuwa utoaji wa elimu ya sheria ni muhimu katika kujenga jamii inayotambua haki zake, kuheshimu sheria na kutumia mifumo rasmi ya utatuzi wa migogoro.




Post a Comment

0 Comments

WANANCHI ZAIDI YA 1,000 WANUFAIKA NA HUDUMA ZA KISHERIA SABASABA