Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
KATIKA jitihada za kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa makazi bora, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa vijana huku ukitangaza fursa 149 za uwekezaji zinazolenga kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.
Pia TBA inawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutembelea banda la TBA ili kujionea fursa zilizopo na kuanza kushirikiana na wakala huo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji ni Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Arusha, Mbeya na Songwe ambapo Dodoma pekee wakala huo unamiliki zaidi ya hekta 630 zinazofaa kwa maendeleo ya nyumba za makazi, biashara, viwanja vya michezo na huduma nyingine za kijamii.
Hayo yameelezwa Julai 7,2026 na Afisa Uhusiano wa TBA, Renatus Sona, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), amesema taasisi hiyo ipo chini ya Wizara ya Ujenzi ina jukumu la kusimamia na kuendeleza mali za Serikali zikiwemo majengo ya ofisi, nyumba za makazi, mashamba na viwanja vya Serikali kwa ufanisi na tija.
Amesema kufuatia uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwaka 2025, TBA imeanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu unaolenga kuwasaidia wananchi, hasa vijana wanaoanza maisha ya ajira, kupata makazi bora yanayolingana na uwezo wao wa kifedha.
Sona amesema mradi huo umeanza katika eneo la Temeke, jijini Dar es Salaam, ambapo zinajengwa nyumba za kisasa za aina mbalimbali zikiwemo za nyumba za chumba kimoja na sebule pamoja maarufu Studio na nyumba za vyumba viwili na sebule.
Amefafanua kuwa nyumba hizo zimezingatia viwango vya kisasa vya makazi na zinajumuisha huduma muhimu kama sehemu ya kupikia, choo na bafu, veranda, eneo la mapumziko pamoja na vyumba vya kulala kulingana na aina ya nyumba husika.
"Lengo letu ni kuwapa vijana makazi bora kwa gharama nafuu ili waweze kupunguza mzigo wa kodi za nyumba, kuokoa fedha na hatimaye kujijengea uwezo wa kumiliki nyumba zao wenyewe," amesema.
Aidha, amesema TBA inaendelea kutekeleza miradi kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia mfumo wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP), hatua inayolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukuza uchumi shirikishi.
Akizungumzia uwekezaji, Sona amesema TBA imebaini maeneo 149 yenye fursa mbalimbali za uwekezaji nchini, huku maeneo 38 yaliyopo katika mikoa 20 tayari yakiwa yameandaliwa kwa ajili ya kuanza miradi ya maendeleo.
Sona ameeleza kuwa maeneo hayo yanafaa kwa uwekezaji katika ujenzi wa hoteli, nyumba za makazi, majengo ya biashara, vituo vya ununuzi, maghala, vituo vya usafirishaji na miradi mingine ya kiuchumi.
Sona amesisitiza kuwa TBA itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza upatikanaji wa makazi bora, kuvutia uwekezaji na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake Afisa Majengo kutoka TBA, Stanley Hashim amesema ubunifu katika usanifu wa majengo wa wataalam wa wakala huo ndio sababu ya kuwapokwa mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
Amesema ubunifu katika usanifu wa majengo unapaswa kuzingatia viwango vya kisasa na kufanywa na wataalamu ili kuhakikisha majengo yanakuwa salama, yenye ubora na yanayokidhi mahitaji ya watumiaji.



0 Comments