DAR ES SALAAM
NAIBU Wakili Mkuu wa Serikali, Alice Mtulo amesema ni muhimu watumishi wa Serikali kuendelea kupewa elimu ya haki za binadamu na kufahamu wajibu wao katika utoaji wa huduma kwa wananchi ili wawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha na kulinda haki za binadamu pamoja na utawala bora nchini.
Mtulo ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam Julai 6, 2026.
Akibainisha mchango wa kundi hilo muhimu amesema kuwa watumishi wa umma ndio wanaokutana na wananchi mara kwa mara wakati wa utoaji wa huduma, hivyo ni muhimu wawe na uelewa mzuri kuhusu haki za binadamu na wajibu wao ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia sheria, utu, usawa na misingi ya utawala bora.
“Watumishi wa Serikali wanapaswa kupewa elimu ya haki za binadamu na kufahamu wajibu wao, kwa kuwa wao ndio sura ya Serikali kwa wananchi. Wakiwa na uelewa huo watatoa huduma kwa weledi na kuwa mabalozi wazuri wa haki za binadamu katika jamii,” amesema Mtulo.
Mtulo pia amesema kuwa utoaji wa elimu hiyo utasaidia kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma, kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za Serikali na kuchangia ujenzi wa jamii inayoheshimu haki za binadamu.
Aidha, akielezea umuhimu wa ushiriki wa THBUB katika maonesho hayo, Bi. Monica Mnanka ambaye ni Msemaji wa Tume hiyo na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma, Mawasiliano, Utafiti na Nyaraka amesema THBUB hutumia maonesho na maadhimisho ya kitaifa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za binadamu, wajibu wa raia na misingi ya utawala bora, pamoja na kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusu uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Wananchi wametakiwa kutumia fursa ya kutembelea banda la THBUB kupata huduma zinazotolewa na tume hiyo na namna ya kushiriki katika kuimarisha utawala bora na kulinda haki za binadamu nchini.

0 Comments