TPHPA YAHAMASISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZA KUDHIBITI VISUMBUFU, YAFUNGUA FURSA ZA MASOKO YA NJE

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imewataka wakulima, wafanyabiashara wa mazao na wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF),kama "Sabasaba" ili kujifunza teknolojia za kisasa za kudhibiti visumbufu vya mazao, matumizi salama ya viuatilifu pamoja na taratibu za kufikia masoko ya kimataifa.

Akizungumza katika maonesho hayo, Julai 7,2026 Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, amesema ushiriki wa mamlaka hiyo unalenga kutoa elimu kwa wadau kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa katika kulinda afya ya mimea na kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.

Amesema matumizi ya teknolojia za kisasa katika kudhibiti visumbufu vya mazao huchangia kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kufungua ajira na kuongeza fursa za masoko ndani na nje ya nchi.

Prof.Ndunguru amesema TPHPA ina jukumu la kuhakikisha mazao yanayouzwa katika masoko ya kimataifa yanakidhi viwango vya ubora vinavyohitajika, hivyo wafanyabiashara wanaotaka kuuza mazao nje ya nchi wanaweza kupata miongozo na taratibu zote muhimu katika banda la mamlaka hiyo.

Amebainisha kuwa hivi karibuni Tanzania imefanikiwa kufungua soko la ndizi mbichi nchini Afrika Kusini, sambamba na soko jingine la mazao 10 katika nchi nyingine, yakiwemo tangawizi, vitunguu, vitunguu saumu na kabichi, hatua inayopanua fursa za biashara kwa wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania.

Aidha, amesema wananchi watapata elimu kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu ili kulinda afya ya walaji, mifugo na mazingira, pamoja na kujifunza teknolojia za udhibiti wa visumbufu kwa njia za kibaolojia kupitia matumizi ya wadudu rafiki na viuatilifu hai vinavyoendelezwa na kituo cha mamlaka kilichopo Kibaha.

Prof.Ndunguru pia ameeleza kuwa TPHPA imeleta huduma za Benki ya Taifa ya Mbegu iliyopo Arusha, ambapo wananchi wanapata fursa ya kufahamu kuhusu hifadhi ya mbegu za asili zinazotumika katika tafiti za kubuni mbegu bora zenye uwezo wa kustahimili ukame, magonjwa na changamoto nyingine za kilimo.

Amewataka wakulima, wafanyabiashara wa mazao na wadau wote wa sekta ya kilimo kutumia maonesho hayo kujifunza teknolojia na huduma zinazotolewa na TPHPA ili kuongeza tija ya uzalishaji na kunufaika na fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.


Post a Comment

0 Comments

WANANCHI ZAIDI YA 1,000 WANUFAIKA NA HUDUMA ZA KISHERIA SABASABA