TOSCI YATOA ELIMU SABASABA KUHUSU UBORA WA MBEGU


Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

MKAGUZI wa mbegu kutoka Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Fatuma Nassoro ameeleza kuwa taasisi hiyo inaendelea kusimamia ubora wa mbegu kuanzia uzalishaji hadi zinapomfikia mkulima huku akiwahimiza wakulima nchini kutumia mbegu zenye ubora uliothibitishwa ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula pamoja na kuongeza kipato.

Hayo ameyasema leo Julai 7,2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF),amesema taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa kufanya ukaguzi,majaribio na uthibitishaji wa ubora wa mbegu zinazozalishwa na kuuzwa nchini.

Amesema TOSCI hukagua maduka ya pembejeo za kilimo, maghala ya kuhifadhia mbegu pamoja na magari yanayosafirisha mbegu ili kuhakikisha ubora wake unaendelea kuzingatiwa kabla ya kumfikia mkulima.

Mkaguzi huyo ameeleza kuwa TOSCI hufanya majaribio ya aina mpya za mbegu, utambuzi wa mbegu, ukaguzi wa mashamba ya wazalishaji wa mbegu pamoja na kutoa mafunzo kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo ili kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora.

"Taasisi hii pia huchukua sampuli za mbegu kutoka kwa wazalishaji na kuzipeleka maabara kwa ajili ya kupima ubora wake, hatua inayosaidia kuhakikisha mbegu zinazouzwa sokoni zinakidhi viwango vinavyotakiwa," amesema.

Akizungumzia ushiriki wao katika Maonesho ya Sabasaba, ameeleza TOSCI inatumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uzalishaji wa mbegu bora, matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo na taratibu za usajili kwa wakulima wanaotaka kujihusisha na uzalishaji wa mbegu.

TOSCI imeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya mbegu namba.l 18 ya mwaka 2003, iliyofanyiwa urekebisho mwaka 2023, kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa sekta ya mbegu na kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zenye viwango vinavyokubalika.

Post a Comment

0 Comments

WANANCHI ZAIDI YA 1,000 WANUFAIKA NA HUDUMA ZA KISHERIA SABASABA