Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limeendelea kuthibitisha nafasi yake si tu katika kuwajenga vijana kwa uzalendo na nidhamu, bali pia katika kuunda fursa za ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi kupitia shughuli za uzalishaji mali zinazoratibiwa na Shirika la SUMAJKT.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 6,2026 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, DkRhimo Nyansaho alipotembelea banda la JKT, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Dk. Nyansaho amesema SUMAJKT imeendelea kuwa mfano wa taasisi ya Umma inayotekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia ajira na kushiriki katika uzalishaji wa bidhaa pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali.
Waziri huyo ameeleza kuwa kampuni tanzu za shirika hilo zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, huku zikitoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.
Hata hivyo ametaja miongoni mwa kampuni hizo kampuni ya Usafi na Unyunyizi Dawa ya SUMAJKT (SUMAJKT Cleaning and Fumigation Company Limited) imefanikiwa kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 4,000 wa Kitanzania.
"JKT kupitia SUMAJKT limeendelea kuonyesha kuwa taasisi za umma zinaweza kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na utoaji wa ajira kwa vijana, jambo linalosaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini," ameema Dk. Nyansaho.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewapongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na JKT kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kulinda usalama wa Taifa sambamba na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.
Ameongeza kuwa mchango wa majeshi hayo unaendelea kuimarisha usalama wa nchi na kuweka mazingira wezeshi yanayowaruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo kwa amani na utulivu.
Aidha, Dk. Nyansaho amewahamasisha wananchi kutembelea banda la JKT katika maonesho hayo ili kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na jeshi hilo kupitia vikosi, makambi, shule, chuo pamoja na huduma na bidhaa zinazotolewa na kampuni tanzu za SUMAJKT.



0 Comments