WAZIRI OMAR APONGEZA MCHANGO WA SELF FM KATIKA UWEZESHAJI WA WANANCHI

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM 

WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameipongeza Mfuko wa SELF Microfinance Fund kwa mchango wake katika kuongeza upatikanaji wa huduma za mikopo kwa makundi mbalimbali ya wananchi, hatua inayochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya wananchi.

Balozi Omar ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la SELF leo Julai 2, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, ambapo amesema mfuko huo umeendelea kutekeleza kwa ufanisi jukumu la kutoa elimu ya masuala ya fedha pamoja na huduma za mikopo na bima.

SELF Microfinance Fund ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha inayotoa huduma za mikopo, bima na elimu ya fedha kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Akitoa maelezo kuhusu shughuli za mfuko huo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Masoko wa SELF FM, Petro Mattaba, amesema huduma kuu zinazotolewa ni mikopo kwa taasisi za huduma ndogo za fedha pamoja na mikopo ya moja kwa moja kwa wanufaika.

Amesema mikopo inayotolewa kwa taasisi za huduma ndogo za fedha hulenga kuzifikia jamii ambazo mfuko hauwezi kuzifikia moja kwa moja, hivyo taasisi hizo huwafikishia wananchi huduma za kifedha kwa urahisi zaidi.

Mattaba amesema walengwa wa mikopo ya moja kwa moja ni pamoja na watumishi wa umma, wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakulima, wafugaji na wavuvi.

Aliongeza kuwa SELF ina matawi 12 Tanzania Bara na tawi moja Zanzibar, hali inayorahisisha wananchi kupata huduma za mikopo, bima na ushauri wa kifedha karibu na maeneo yao.

"Aidha, tupo hapa Sabasaba kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na SELF, ikiwemo mikopo, bima na elimu ya fedha, ili waweze kuzitumia fursa hizi kuboresha maisha yao," amesema Mattaba.

Amesema SELF pia ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika utekelezaji wa programu za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi, zikiwemo programu za mikopo kwa vijana, wanawake na makundi mengine maalumu.

Mattaba amesema mwaka 2025 mfuko huo ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 43 iliyowanufaisha zaidi ya wananchi 38,000 nchini, ambapo zaidi ya asilimia 51 ya wanufaika hao walikuwa wanawake.

Ameongeza kuwa mfuko huo unaendelea kuwezesha taasisi za huduma ndogo za fedha kwa kuzipatia mikopo yenye riba nafuu ili nazo ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan walioko maeneo ya vijijini na ambao hawana huduma za kifedha kwa urahisi.

Amewahimiza wananchi kutembelea banda la SELF katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na mfuko huo pamoja na kufahamu fursa mbalimbali za mikopo zinazoweza kuwasaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments

WAZIRI OMAR APONGEZA MCHANGO WA SELF FM  KATIKA UWEZESHAJI WA WANANCHI