DIB YATOA UHAKIKA WA FIDIA,WANANCHI WAHIMIZWA KUENDELEA KUWEKA AKIBA


 Na Asha Mwakyonde,DODOMA

BODI ya Bima ya Amana (DIB), imewahakikishia wananchi kuwa amana zao katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ziko salama, ikieleza kuwa kila mteja analindwa kwa kiwango cha hadi shilingi milioni 7.5 endapo benki itafilisika au kufutiwa leseni. 

Hatua hiyo imelenga kuimarisha imani ya wananchi katika sekta ya fedha na kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba kwa uhakika, huku DIB ikiendelea kutoa elimu kwa umma kupitia Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.

Akizungumza leo Agosti 6, 2026 katika maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, amesema kiwango hicho cha bima ya amana kinamaanisha kuwa mteja mwenye amana zisizozidi shilingi milioni 7.5 atalipwa fedha zake zote ikiwa benki anayohifadhi fedha zake itashindwa kuendelea na shughuli zake kutokana na kufilisika au kufutiwa leseni.

Amesema mfuko wa bima ya amana huchangiwa na benki pamoja na taasisi za fedha zinazopokea amana kutoka kwa wananchi, ambapo kila taasisi huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana zake mara moja kwa mwaka.

Mwambande ameeleza kuwa fedha zinazokusanywa katika mfuko huo huwekezwa kwenye dhamana za Serikali na maeneo mengine salama ya uwekezaji ili kuhakikisha DIB inakuwa na uwezo wa kulipa fidia kwa wateja pale benki inaposhindwa kuendelea na shughuli zake.

Aidha, amesema kwa sasa Bodi inaendesha ufilisi wa benki tisa zilizofungwa kati ya mwaka 2000 na 2018 ambazo ni Greenland Bank, Delphis Bank, FBME Bank, Efatha Bank, Covenant Bank for Women, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank na Kagera Farmers Cooperative Bank.

Kwa upande wake, Meneja wa Fedha na Uhasibu wa DIB, Romuli Mtui, amesema mchakato wa ufilisi wa benki saba zilizofungwa mwaka 2017 na 2018 bado unaendelea katika hatua mbalimbali kwa kuzingatia taratibu za kisheria, huku Bodi ikiendelea kusimamia maslahi ya wadai na wenye amana kwa uwazi na ufanisi.

Post a Comment

0 Comments

ZAIDI YA WATU 186 WANUFAIKA NA HUDUMA YA KUPUNGUZA UZITO KWA NJIA YA PUTO MLOGANZILA