TIRA YATOA ELIMU YA BIMA YA KILIMO KULINDA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), imeendelea kuhamasisha wakulima na wafugaji nchini kutumia bima ya kilimo ili kujikinga dhidi ya hasara zinazoweza kusababishwa na majanga mbalimbali yanayoathiri uzalishaji wa mazao na mifugo.

Hayo yamesemwa leo Agosti 3, 2026 na Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma kutoka TIRA, Anna Massao, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda la mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dk. John Malecela Nzuguni jijini hapa.

Massao amesema ushiriki wa TIRA katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kuhusu umuhimu wa bima kwa wananchi, huku msisitizo mkubwa ukiwa kwenye bima ya kilimo ambayo imebuniwa kumlinda mkulima na mfugaji dhidi ya hasara zinazoweza kujitokeza wakati wa uzalishaji.

Amefafanua kuwa wakulima wanaweza kukumbwa na majanga mbalimbali kama mvua nyingi, ukame, mafuriko na changamoto nyingine zinazoweza kusababisha mazao kuharibika au kushindwa kuvunwa, huku bima ya kilimo ikitoa kinga ya kifedha pale hasara inapojitokeza.

Aidha, amesema kwa upande wa mifugo, bima hutoa ulinzi dhidi ya hasara zinazotokana na magonjwa, vifo vya mifugo, wizi na matukio mengine yanayoweza kuathiri shughuli za ufugaji.

Massao ameeleza kuwa katika banda la TIRA wananchi wanapata fursa ya kuonana na kampuni mbalimbali zinazotoa bima ya kilimo, ikiwemo Shirika la Taifa la Bima (NIC), Umoja wa Makampuni ya Bima za Kilimo Tanzania (TAIC), pamoja na kampuni nyingine zinazoshiriki kutoa huduma za bima kwa sekta ya kilimo.

Ameongeza kuwa banda hilo pia linatoa huduma kupitia Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania (Tanzania Insurance Ombudsman), inayoshughulikia malalamiko na migogoro inayohusiana na huduma za bima kwa lengo la kuhakikisha haki inapatikana kwa wateja.

Massao amewaalika wananchi wa Dodoma na mikoa mingine ambako Maonesho ya Nanenane yanaendelea kutembelea banda la TIRA ili kupata elimu kuhusu huduma za bima na namna zinavyoweza kulinda uwekezaji wao katika sekta ya kilimo na mifugo.

Post a Comment

0 Comments

MAHUNDI ASHIRIKI MAPOKEZI YA MWAKILISHI WA MWENYEKITI WA UWT TAIFA KATIKA ZIARA YA KIKAZI CHUNYA