MAHUNDI AONYA VIKWAZO KATIKA UTOAJI WA MIKOPO KWA WANAWAKE








Na Jackline Minja, MBEYA

WANAWAKE wanaotafuta mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara wanapaswa kupata huduma kwa wakati bila kukwamishwa na urasimu usio wa lazima, huku Maafisa Maendeleo ya Jamii wakitakiwa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuwaongoza na kuwasaidia kukamilisha taratibu za mikopo.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani Mbeya, Novemba 12, 2026.

Mahundi amesema Maafisa Maendeleo ya Jamii wana jukumu muhimu la kuhakikisha wanawake wanapata mikopo na fursa nyingine za kiuchumi kwa urahisi, hivyo wanapaswa kuwa karibu nao, kutoa maelekezo sahihi na kuwasaidia katika hatua mbalimbali za maombi ya mikopo.

Amesisitiza kuwa makongamano ya uwezeshaji wanawake hayapaswi kuwa shughuli za kawaida za kukutana, bali yawe majukwaa ya kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi na kuimarisha uwajibikaji katika utoaji wa huduma.

"Tusifanye haya makongamano kama fasheni, yawe njia nzuri ya kukumbushana kuwahudumia wananchi. Tuache longolongo," amesema Mahundi.

Amefafanua kuwa uwezeshaji wanawake kiuchumi unahusisha kuwapatia fursa, rasilimali, ujuzi, mitaji na teknolojia ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za biashara, kilimo, viwanda na sekta nyingine zinazozalisha kipato.

Aidha, amesema licha ya hatua zilizopigwa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, bado wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mikopo, mitaji na mazingira rafiki ya kufanya biashara, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na wadau kuimarisha mifumo ya kifedha.

Akizungumzia umuhimu wa kuwawezesha wanawake mkoani humo, Mahundi ametumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinazoonesha kuwa wanawake ni asilimia 52 ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya, sawa na watu 1,219,926.


Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuweka mazingira yatakayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amesema elimu inayotolewa kwa wanawake kuhusu uwezeshaji kiuchumi ni muhimu katika kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Mbeya, Neema Kisanga, akiwasilisha risala, amewasilisha maoni ya jukwaa kuhusu umuhimu wa kuendeleza juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.

Kongamano hilo limewakutanisha viongozi, wadau na wanawake wajasiriamali kujadili fursa, mafanikio na changamoto zinazowakabili wanawake katika shughuli za kiuchumi, pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.



Post a Comment

0 Comments

MAHUNDI AONYA VIKWAZO KATIKA UTOAJI WA MIKOPO KWA WANAWAKE